Majadiliano ya kidini ni muhimu katika kulinda, kukuza na kutetea haki msingi za binadamu,
amani na mshikamano wa kitaifa!
Visiwa vya Zanzibar ni mlango wa Imani ya Kanisa Katoliki Afrika Mashariki. Hii inatokana
na juhudi zilizofanywa na Wamissionari wa Roho Mtakatifu yapata miaka 150 iliyopita.
Juhudi za Wamissionari
hawa zilipania pamoja na mambo mengine kukomesha biashara ya utumwa sanjari na kuwajengea
wananchi uwezo wa kupambana na mazingira yao kwa njia ya elimu. Majadiliano ya
kidini kati ya Waislam na Wakristo Visiwani Zanzibar ni jambo la kihistoria tangu
wakati wa utawala wa Sultan Sayyid Barghash aliyeruhusu ujenzi wa Kanisa katika eneo
la Mji Mkongwe, Kanisa la Minara miwili. Waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo waliishi
pamoja na kuheshimiana kama ndugu hata katika tofauti za imani na tamaduni zao. Askofu
Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar anasema, hali ya amani, utulivu na uhuru
wa kuabudu vinaanza kumong’onyoka taratibu Visiwani Zanzibar kutokana na kuibuka kwa
chuki za kidini zinazofanywa na waamini wenye misimamo mikali ya kiimani. Chuki na
uhasama huu kama havitaweza kudhibitiwa kikamilifu na vyombo vinavyohusika, maafa
yake ni makubwa. Kumbe, kuna haja ya kuendeleza utamaduni wa majadiliano ya kidini,
hali ya kuvumiliana, kuheshimiana na kusaidiana kama ndugu bila ya kuwepo kwa misingi
ya ubaguzi unaoendekezwa kwa misingi ya udini. Waislam na Wakristo ni wakazi wa Zanzibar
na wote wana haki ya kuendelea kuishi Zanzibar. Askofu Shao anasema kwamba, chuki
za kidini na ubaguzi dhidi ya Wakristo ni jambo ambalo limepandikizwa, kwa ajili ya
mafao ya watu wachache wasiowatakia mema wananchi wa Zanzibar katika ujumla wao. Hakuna
uhusiano wowote kati ya Muungano na Kanisa; kwani siasa zinafanywa na wanasiasa na
Kanisa linahubiri Habari Njema ya Wokovu, mambo mawili tofauti kabisa! Madhulumu ya
viongozi wa Kanisa katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani Visiwani Zanzibar imekuwa
ni changamoto kubwa kwa waamini kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani
yao kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu! Ubaguzi na madhulumu
ya kidini yasipodhibitiwa kwa ukamilifu, Zanzibar inaweza kujikuta ikitumbukia katika
maafa na kuharibu jina zuri la Visiwa vya Zanzibar katika ramani ya dunia. Watu wachache
wenye nia mbaya wasiruhusu kuvuruga amani, upendo na mshikamano wa kitaifa Zanzibar.
Watu wajenge moyo na utamaduni wa kujadiliana, kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana.
Uhuru wa kidini ni kati ya haki msingi za binadamu, uheshimiwe na kulindwa na vyombo
husika. Matukio ya kuchomwa moto kwa Makanisa, kushambuliwa kwa viongozi wa kidini
ni kati ya mambo yanayoendelea kuwatia hofu wananchi wengi Visiwani Zanzibar. Mwaka
wa Imani iwe ni fursa ya kuimarisha imani, matumaini na mapendo miongoni mwa waamini
na watu wote wenye mapenzi mema Visiwani Zanzibar.