2013-11-05 11:00:09

Kipigo kwa wanawake ni jambo lililopitwa na wakati, Jamii ijenge utamaduni wa kuheshimu na kuwathamini wanawake!


Wajumbe wa mkutano mkuu wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wanasema kwamba, umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, uonevu, nyanyaso, dhuluma na ubaguzi dhidi ya wanawake vinakomeshwa na badala yake haki msingi za binadamu zinatawala miongoni mwa Jamii. RealAudioMP3

Wajumbe wanabainisha kwamba, kwa miaka mingi wanawake wameendelea kubaguliwa na kudhulumiwa haki zao msingi ndani ya Jamii, jambo ambalo haliwezi kuruhusiwa kuendelea hata katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Baraza la Makanisa Ulimwenguni kati ya Mwaka 1988 hadi Mwaka 1998 liliendesha kampeni iliyolenga kudumisha mshikamano na wanawake, jambo ambalo limezaa matunda mengi katika maisha na utume wa wanawake ndani ya Kanisa.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wanasema, kuna haja kwa Makanisa sehemu mbali mbali za dunia, kuunga mkono juhudi za kualetea wanawake ukombozi wa kweli kwa njia ya elimu pamoja na kuhakikisha kwamba, haki zao msingi zinalindwa na kuheshimiwa na Jamii husika.

Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake, kwa kuhakikisha kwamba, wananchi wanakuwa salama dhidi ya vitisho, dhuluma na nyanyaso bila kusahau utumwa mamboleo unaowatumbukiza wanawake na wasichana katika biashara haramu ya binadamu.

Wajumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wanaendelea kuchambua umuhimu wa kudumisha na kuendeleza haki msingi za binadamu kama njia ya kuenzi zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kauli mbiu inayofanyiwa kazi na wajumbe hao katika mkutano wao mkuu. Waamini na watu wenye mapenzi mema wanaendelea kuhimizwa kulinda na kutunza pia mazingira kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.