2013-11-04 08:35:25

Papa anawaombea faraja Mapadre wanaokabiliana na magumu katika maisha, ili waimarike katika uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake!


Nia ya Baba Mtakatifu kwa Mwezi Novemba 2013 ni kwa ajili ya kuwaombea Mapadre wanaokabiliana na magumu katika maisha, ili waweze kupata faraja katika mateso yao, msaada katika mashaka yao na kuimarishwa katika uaminifu wao. RealAudioMP3

Mwenyeheri Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kichungaji “Pastores Dabo Vobis” anazungumzia kuhusu upweke chanya na hasi wanaokabiliana nao Mapadre katika maisha na utume wao kama ulivyojadiliwa na Mababa wa Sinodi. Anasema upweke chanya ni jambo la kawaida katika maisha ya kikasisi, lakini upweke hasi unasababisha mahangaiko makubwa moyoni.

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na uwajibikaji shirikishi miongoni mwa Makleri wote Jimboni ili kujenga na kuimarisha uhusiano na Askofu mahalia. Makleri wajenge utamaduni wa maisha ya Kijumuiya, kwa kushirikishana, kusaidiana na kutaabikiana kama ndugu katika Kristo. Mapadre wapanie kuimarisha urafiki mwema na waamini walei ambao ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa maparokiani.

Zote hizi ni njia makini zinazoweza kuwasaidia Makleri kuondokana na upweke hasi, wanaoweza kukumbana nao katika maisha na utume wao kama Mapadre. Upweke unaweza kuwa ni mwanzo wa mchakato wa fursa mbali mbali katika maisha na utume wa Makleri, kama utapokelewa kwa moyo wa unyenyekevu. Hii ni nafasi ya kujenga uhusiano wa karibu zaidi na Yesu Kristo, kwa njia ya sala na tafakari ya Neno la Mungu.

Mambo haya yakipewa msukumo wa pekee, unaweza kuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa maisha ya utakatifu na ukuaji wa kiutu. Ikumbukwe kwamba, hata Yesu mwenyewe katika maisha yake, alijitahidi kutafuta muda wa kukaa peke yake mbele ya Baba yake akisali.

Makleri wajijengee uwezo wa kudhibiti upweke unaotokana na myumbo wa afya, ili kupata utulivu wa maisha ya kiroho. Katika upweke wao, wajaribu daima kuwa na karibu na Kristo anayewafariji, kwani kwa nguvu zao binafsi watashindwa na kuteseka zaidi.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili anasema, Makleri wazee wanateseka sana kutokana na upweke, hali ambayo inaweza kuwa ni hatari kubwa katika maisha yao. Ni watu wanaoweza kukata tamaa wanapoangalia historia ya maisha yao. Uzee iwe ni sehemu ya mchakato wa majiundo endelevu katika maisha ya Makleri na utume wao kwa Kanisa. Makleri waendelee kukesha wakiwa na tumaini la maisha ya uzima wa milele, daima watambue kwamba, wao ni “Watu wa Mungu”.

Majandokasisi wanaojiandaa kwa maisha na utume wa Kipadre wanachangamotishwa kutokata tamaa katika hija ya majiundo yao; wawe ni watu wenye furaha, imani na matumaini ya kuweza kuwahudumia waamini kwa moyo na akili zao zote.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, imani, matumaini na mapendo yanakuwa na kukomaa miongoni mwa watu wa nyakati hizi. Makleri wote watambue kwamba, wito wao wa Kipadre ni hazina kubwa iliyohifadhiwa kwenye vyombo vya udongo kama anavyosema Mtakatifu Paulo kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kristo. Majiundo endelevu ni jambo ambalo linapaswa kupewa msukumo wa pekee katika maisha ya Kipadre. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza Makleri wote kwa maisha na utume wao ndani ya Kanisa.

Nia za Kimissionari za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Novemba, 2013 ni ili kwamba, kama sehemu ya matunda ya utume, Makanisa ya Amerika ya Kusini yaweze kutuma Wamissionari kwa Makanisa mengine. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alipokuwa anazungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil kunako mwezi Mei, 2007, alisema kwamba, Kanisa bado linachangamotishwa kujikita katika Uinjilishaji shirikishi unaowahusisha watu wengi zaidi.

Hawa ndiyo Wamissionari wanaotekeleza wajibu wao katika mazingira magumu, ili kueneza ukweli wa Kiinjili. Ili utume huu uweze kufanikiwa kuna haja ya kuendelea kushirikiana na wadau mbali mbali katika azma ya Uinjilishaji Mpya, daima wakijitahidi kujenga na kuimarisha mshikamano na viongozi wao wa Kanisa, ili kuwashirikisha wengine utajiri wa maisha ya kimissionari unaofumbatwa katika moyo wa Kanisa, kielelezo makini cha utajiri wa maisha ya Kikristo.

Kazi ya kimissionari inawaguse na kuwahusisha watu wengi zaidi, watakaoweza kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Ni watu wanaopaswa kujikita katika Kristo na Kanisa lake, ili kweli waweze kuwaimarisha ndugu zao katika imani kwa Kristo na Kanisa lake bila kuyumba wala kuwayumbisha wengine.

Wawe ni waamini wenye imani thabiti, waliobahatika kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao anayewapatia mwelekeo mpya wa maisha. Waamini wajenge na kuimarisha uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake, kamwe wasiwe ni watu wanaotangatanga na kuyumbishwa katika misingi ya imani yao. Kanisa ni mahali makini pa kuweza kukutana na Yesu kwa njia ya Katekesi makini; maisha ya sala na huduma ya upendo.

Umaskini wa watu wengi, kimekuwa ni kikwazo cha wengi kutaka kulikimbia Kanisa Katoliki kwa kudhani kwamba, huko wanakokimbilia wataweza kupata nafuu ya maisha kwa njia ya miujiza. Kanisa lijiwekee mikakati ya kuwasaidia watu kiroho na kimwili, kwa kuonesha mshikamano wa upendo.

Kanisa lisimame kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, ili haki na amani viweze kushamiri kati ya watu. Maaskofu wawe ni mfano wa wachungaji wema, wanaosimamia kwa umakini mkubwa Neno la Mungu, Mafumbo ya Kanisa na Huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Nia hizi zimetayarishwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.,
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.