Mkate, akili, elimu na umaskini ni tema zinazokwenda pamoja katika maisha ya mwanadamu!
Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani katika hotuba yake
ya ufunguzi wa mkutano wa Kikosi kazi cha Baraza la Kipapa la Taasisi za Sayansi,
Jumatatu tarehe 4 Novemba 2013 anabainisha kwamba, "Mkate, Akili, Elimu na Umaskini"
ni mambo yanayokwenda pamoja, kiasi cha kuwatumbukiza mamillioni ya watu katika lindi
la umaskini, ujinga, njaa na utapiamlo wa kutisha
Mwili unaopata lishe bora
unakuwa na afya njema ya akili na roho na kwamba, elimu ni chakula cha akili ya mwanadamu.
Mada zinazojadiliwa na kikosi kazi katika mkutano wake zinarandana na Malengo ya Maendeleo
ya Millenia, ifikapo Mwaka 2015; yanayopania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba,
Jumuiya ya Kimataifa inafutilia mbali umaskini, ujinga na baa la njaa na kwamba, watoto
wengi zaidi wanapata fursa ya elimu ya msingi. Watoto wanaopata chakula shuleni wameonesha
mafanikio makubwa katika sekta ya elimu katika nchi zinazoendelea duniani.
Kardinali
Turkson anasema kwamba, kuna haja kwa akili na mwili kulishwa vyema kwa njia tafiti
makini za kisayansi sanjari na matumizi bora ya sayansi na teknolojia itakayomwezesha
mwanadamu kuzalisha chakula na lishe ya kutosha pamoja na kumjengea mwanadamu uwezo
wa kupambana na baa la umaskini duniani, kama njia ya kuinua utu na heshima ya binadamu,
kwani haya ni mambo yanayogusa haki, amani na utulivu kama ambavyo alikwisha wahi
kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.
Lishe duni ya akili
na mwili ni hatari kubwa kwa maisha ya mwanadamu; jambo linalopaswa kushughulikiwa
kisayansi pamoja na sera makini zinazolenga maboresho katika sekta ya elimu, usalama
na uhakika wa chakula kwa kuzingatia: uzalishaji, usambazaji pamoja na kuweka mikakati
ya kilimo bora na endelevu; kwa kuongozwa na kanuni ya mshikamano na udugu.
Mchakato
huu unahitaji majadiliano ya kina, ili kila upande uweze kuchangia mawazo na mikakati
yake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu. Majadiliano yatumike kubainisha
vikwazo na vizingiti katika mapambano dhidi ya baa la njaa, umaskini na ujinga duniani
ili kujenga mshikamano wa kidugu! Kila mwamini anachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha
kwamba, anashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya baa la njaa ili kila mtu aweze
kupata riziki yake ya kila siku.
Waamini na watu wenye mapenzi mema, wasimame
kidete kulinda na kutetea haki msingi za maskini pamoja na kushiriki katika ujenzi
wa Jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na amani.