Kituko cha Zakayo tajiri na fisadi ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani, ili
kukumbatia amani, furaha na wokovu!
Umati mkubwa wa waamini na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Jumapili iliyopita,
tarehe 3 Novemba 2013 walikusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
ili kusali na kutafakari pamoja na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika
wa Bwana.
Baba Mtakatifu anasema, sehemu ya Injili ya Jumapili ya 31 ya Mwaka
wa C wa Kanisa, inaonesha sehemu ya mwisho ya hija ya maisha na utume wa Yesu hapa
duniani, inayopania kuwaokoa wanakondoo wa nyumba ya Israel waliopotea, utume unaoendelea
kumwongezea maadui. Mwinjili Luka, anamwonesha Zakayo, tajiri na mkuu wa watoza ushuru;
fisadi na mwizi wa kodi. Haya ni kati ya mambo yaliyopelekea Zakayo kushindwa kumwona
Yesu uso kwa uso, kiasi cha kuparamia na kukwea juu ya mti ili aweze kumwona Yesu.
Yesu
anapofika mahali pale, anayainua macho yake na kumwambia Zakayo ashuke upesi kwani
Yesu alitamani kukaa naye nyumbani mwake. Yesu anamwita Zakayo kwa jina yule ambaye
alionekana mfupi wa kimo kuliko wote, mtu ambaye alikuwa haonekani, lakini mbele ya
Yesu anapata kipaumbele cha pekee! Huyu ndiye Zakayo, maana yake, "Mungu anakumbuka".
Yesu anaamua kuingia na kukaa nyumbani kwa Zakayo, hali inayozua chuki na uhasama
kati ya watu kwa kumshutumu Yesu kwamba, alikuwa anakaa na kula na wadhambi.
Baba
Mtakatifu anasema, uwepo wa Yesu nyumbani kwa Zakayo unaleta: amani, furaha na wokovu.
Hii ni kumbukumbu hai ya huruma na upendo wa Mungu kwa wadhambi na hakuna dhambi au
tendo ambalo linaweza kufutilia mbali huruma na upendo wa Mungu kwani wao wameumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu. Daima anaendelea kusubiri kwa uvulimivu kuwaona watoto
wake wakimrudia kwa toba na wongofu wa ndani, ili aweze kuwaonjesha upendo na huruma
yake isiyokuwa na kifani.
Kitendo cha Zakayo tajiri na mkuu wa watoza ushuru
kinawashangaza wengi, lakini ni kielelezo cha wokovu, changamoto na mwaliko kwa kila
mwamini kuchunguza dhamiri yake mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kuonja uwepo endelevu
wa Mungu katika hija ya maisha yake, Mungu ambaye yuko tayari kuwapokea na kuwakumbatia
kama alivyofanya Yesu kwa Zakayo mtoza ushuru. Yesu mwingi wa huruma na mapendo, daima
yuko tayari kusamehe na kusahau; bado anaendelea kuwaita watu kwa majina, jambo la
msingi na kusikiliza kwa makini sauti yake na kuipokea kwa moyo wa furaha.
Kwa
njia ya Kristo hata mdhambi aliyejikatia tamaa anaweza kutubu na kumwongokea Mungu;
anaweza kumwokoa mwamini kutoka katika ubinafsi wake na kumkirimia zawadi ya upendo!
Baba Mtakatifu alihitimisha tafakari yake kwa kuwasalimia na kuwatakia wote kheri
na baraka zake za kitume.