Kikosi kazi cha Baraza la Kipapa la Taasisi za Kisayansi chaanza mkutano wake unaoongozwa
na kauli mbiu "Mkate na Akili"
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 4 Novemba 2013 amekutana na washiriki wa
mkutano wa kikosi kazi cha Baraza ya Kipapa la taasisi za Kisayansi na kupiga nao
picha kwenye makazi yake ya muda ya Hosteli ya Mtakatifu Martha, mjini Vatican. Mkutano
wa Kikosi kazi unatarajiwa kufungwa hapo tarehe 6 Novemba 2013.
Baraza hili
la kipapa linautajiri mkubwa wa historia ya mikutano inayounganisha mabaraza na taasisi
mbali mbali za kipapa, ili kuweza kujadili changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu
wa utandawazi mintarafu elimu na umaskini wa watu. Lengo la mkutano wa kikosi kazi
ni kuibua mbinu mkakati utakaotumiwa na wengi katika mchakato wa maboresho ya maisha
ya mwanadamu, ili kumwongezea matumaini zaidi.
Mkutano huu unaongozwa na kauli
mbiu "Mkate na Akili", kwa kufanya rejea inayogusa maendeleo ya sayansi na teknolojia
ili kuleta maboresho ya chakula na lishe sanjari na mapambano dhidi ya baa la njaa
na utapiamlo; mambo ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa ubora wa elimu
hususan katika nchi zinazoendelea duniani.
Jumuiya ya Kimataifa imepiga hatua
kubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, mambo yanayoweza kusaidia katika
mapambano dhidi ya baa la njaa na lishe duni sanjari na maboresho ya sekta ya elimu
kwa mamillioni ya watu katika nchi zinazoendelea duniani, ili kuinua utu na heshima
yao; tayari kushiriki katika mikakati ya kujiletea maendeleo endelevu.
Kikosi
kazi, kimegawanyika katika makundi makuu manne yanayopembua vinasaba vya mimea, ukuaji
wa akili ya mwanadamu, usalama wa chakula na elimu kama sehemu ya mchakato wa ukuaji
wa mtui mzima: kiroho na kimwili pamoja na kuangalia changamoto za kimaadili zinazoendelea
kujitokeza.