Baba Mtakatifu atembelea na kusali kwenye Makaburi ya watangulizi wake, yaliyoko chini
ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
Katika Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Marehemu wote, Jumamosi, tarehe 2 Novemba 2013,
majira ya jioni, Baba Mtakatifu Francisko alitembelea makaburi ya watangulizi wake
waliozikwa chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hija hii ya sala
na maisha ya kiroho ilianzia kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, mwamba wa imani Baadaye,
Baba Mtakatifu alipita na kusali mbele ya baadhi ya Makaburi kwa kitambo kidogo.
Baba
Mtakatifu katika sala yake, amewaweka watangulizi wake waliolazwa kwenye Makaburi
yaliyoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu, wakiwa na tumaini la ufufuko na maisha
ya uzima wa milele. Kwa namna ya pekee, amewakumbuka Mapapa ambao walijitosa kimasomaso
kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kiulimwengu, ili waweze kushiriki katika liturujia
ya mbinguni.
Hili ndilo tumaini la Mama Kanisa lisilochakaa wala kupitwa na
wakati, wakati huu Kanisa linapowaombea watoto wake huruma ili waweze kushirikishwa
katika makazo ya Yerusalem ya mbinguni.