Kila mmoja anapaswa kutua vyema Nanga ya moyo wake mahali pazuri panapofaa..
Papa Francisko Ijumaa jioni aliongoza Ibada ya Misa, akiwa katika lango la Makaburi
ya Verano Roma, kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Watakatifu wote, na baadaye kuwaombea
wahamiaji marehemu wote waliofariki jangwani au baharini, wakati wakiwa katika harakati
za kutafuta maisha mapya. Ibada hii ya Misa ya Kipapa ilifanyika katika eneo
hilo la Makaburi ya kihistoria kwa jiji la Roma, baada ya kupita miaka 20 tangu Papa
Yohane Paulo II alipofanya ibada kama hiyo Novemba Mosi, 1993. Papa Francisko
katika hotuba yake alisema, “mawazo yetu na yawaendee wale walio tutangulia na ambao
sasa wako mbinguni pamoja na Bwana. Papa alionyesha imani yake kwamba wapo kwa sababu
waliokolewa na Kristo . Na si tu waliokolewa kwa sababu ya matendo yao mema, lakini
ni kutokana na imani yao kwa Kristu iliyowawezesha kuyafuata maagizo ya Mwokozi wao
na kumpenda.
Mahali hapo Papa alikumbusha wote kwamba, tunaweza tu kuingia
katika mlango wa mbinguni kwa damu yake Kristo. Ni Yeye ndiye atakaye tuhukumu
na ndiye atakaye fungua mlango wa mbinguni. Hili ni tumaini letu, aliendelea, iwapo
tutaendelea kutembea katika njia ya Kristo, tukidumu katika tumaini hili na kukubali
kuandamana naye, naye kamwe hawezi kututelekeza.
Papa alieleza na kuwakumbuka
Wakristu wa mwanzo ambao waliliweka tumaini kuwa nguzo ya maisha yao. Tumaini la
moyo, ,lililosimikwa katika nanga ya wapendwa wetu waasisi , ambao sasa ni Watakatifu
wako mahali ambako Kristo yuko na ambapo Mungu yuko. Hili ndilo tumaini letu alisisitiza
Papa Francisko.
Kila mmoja wetu katika siku hizi , Papa aliendelea, anapaswa
kufikiri juu ya mwisho wa maisha yake. Ni lazima kuangalia mbele kwa matumaini
na furaha ya kupokelewa na Bwana.Ni lazima tujiulize , mahali tulipoweka nanga ya
moyo wetu , na kuhakikisha kwamba nanga hiyo imetua vizuri katika pwani ya maisha
.
Papa alikamilisha ibada hii kwa kuwakumbuka Marehemu wote waliofariki jangwani
au bahari wakati wakihangaika kutafuta njia mpya za kuwa na maishayaliyo bora zaidi.