Wanafunzi 468 kutoka katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mwenge, MWUCE, kilichoko
mjini Moshi, Kilimanjaro nchini Tanzania, Jumamosi tarehe 2 Novemba 2013 wanatarajiwa
kutunukiwa shahada ya kwanza, shahada ya uzamili, diploma na cheti katika masomo mbali
mbali yanayotolewa Chuoni hapo.
Haya ni mahafali ya sita, tangu Chuo hiki
kilipofunguliwa kama jitihada za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kushiriki kikamilifu
katika mchakato wa maboresho ya sekta ya elimu nchini Tanzania. Hii ni elimu inayopania
kumletea mwanadamu ukombozi kamili: kiroho na kimwili. Elimu inayotolewa Chuoni hapo
inapania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, mwanafunzi anapata ujuzi na maarifa
katika kusoma na kufundisha; kufanya tafiti na kuzichapisha pamoja na kuendelea kushiriki
katika utoaji wa huduma ndani na nje ya Tanzania.
MWUCE kinapania kuwa ni Chuo
Kikuu kitakachoongoza mchakato wa kufundisha, kusoma pamoja na kufanya tafiti kwa
ajili ya kuwaandaa wanafunzi watakaotoa huduma kwa ngazi na mahitaji mbali mbali ya
Jumuiya ya Kitaifa na Kimataifa. Hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba, wahitimu wa
MUCE wanaiva barabara kitaaluma, daima wakitambua kwamba, kama raia wanawajibika kushiriki
kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya watu wao, kwani wanatumwa kuwa ni Mwanga
wa Dunia "Lux Mundi".
Chuo pamoja na mambo mengine kinakazia: uaminifu, usawa
na tunu msingi za kimaadili na utu wema. Uwajibijaki, ukweli na uwazi; umoja na ushirikiano
kama timu katika utekelezaji wa mipango na mikakati ya elimu Chuoni hapo. Kila mdau
wa MWUCE anafursa sawa katika kujitafutia maendeleo yake kwa kuzingatia sheria na
kanuni za Chuo.