Sekretarieti ya Papa itakuwa na uwezo wa kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza
wajibu wake kwa Kanisa la Kristo!
Askofu mkuu Pietro Parolin amerejea mjini Roma, tayari kwa maandalizi ya utume wake
mpya kama Katibu mkuu wa Vatican dhamana aliyopewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa
mshangao mkubwa na bila hata masitahili yake. Anasema, ameanza maisha haya mapya,
taratibu, ingawa anakiri kwamba, walau anao uzoefu na mang'amuzi ya utume huu mpya
kwani aliwahi kufanya kazi kwenye Sekretarieti ya Vatican kabla ya kuteuliwa kuwa
Balozi wa Vatican nchini Venezuela.
Askofu mkuu Parolin mwenye umri wa miaka
58 anasema, kunako mwaka 1992 aliteuliwa kufanya kazi kwenye Sekretarieti ya Vatican,
sehemu ya pili. Mwaka 2000 alihamishiwa kwenye kitengo cha mashauri ya kichungaji
kwa watawa na wahudumu wa maisha ya kiroho magerezani na hospitalini. Kunako mwaka
2002 akateuliwa kuwa ni Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican, utume alioutekeleza hadi mwaka 2009 alipoteuliwa na Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kuwa Balozi wa Vatican nchini Venezuela.
Askofu
Marcello Semeraro, Katibu wa Jopo la Makardinali wanane lililoteuliwa na Baba Mtakatifu
Francsiko kusaidia kutoa ushauri wa magezi yaliyotolewa na Makardinali anasema kwamba,
kati ya mabadiliko yanayotarajiwa ni muundo ambao utaitwa "Sekretarieti ya Papa" kwani
jina Katibu mkuu wa Vatican linaweza kuwapotosha watu kwani linaharufu kubwa ya mambo
ya kisiasa kuliko hata maisha ya kiroho. Sekretarieti ya Papa inapania kumsaidia Baba
Mtakatifu kutekeleza wajibu na dhamana yake kama Askofu wa Roma na Khalifa wa Mtakatifu
Petro, kwa kuzingatia uelewa makini wa Kanisa.
Sekretarieti ya Papa itakuwa
na wajibu wa kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza wajibu na dhamana yake
ya uongozi wa Kanisa la Kiulimwengu, kama ilivyofafanuliwa hivi karibuni na Padre
Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican.