Ninakualika katika tafakari yetu tukiwakumbuka marehemu wote. Kila mwaka tarehe 2
Novemba na zaidi sana mwezi Novemba ni siku na wakati ambao Mama Kanisa anatualika
kwa ajili ya kuwaombea marehemu walioko toharani.
Kwa kawaida siku zote Mama
Kanisa anasali kwa ajili ya marehemu mmojammoja au kikundi lakini leo anasali kwa
ajili ya Kanisa zima la wateswa lililoko toharani. Huo ndio utajiri wa kanisa linapogawa
mastahili ya msalaba wa Kristu kwa wahitaji walioko safarini kuelekea mbinguni.
Mwanafalsafa
John Mbiti alisema “Niko kwa sababu tuko na kwa vile tuko, kwa hiyo niko” Sentesi
hii yanitafakarisha na kunisaidia kuhisi uwapo wa mwingine pembeni mwangu aliye mhitaji
na hivi yaonesha hitaji la jumuiya. Katika siku ya leo Kanisa lahisi uwapo wa wahitaji
ndio marehemu wote, ndio waliolala toharani wakitakaswa ili waingie mbinguni. Kanisa
lahisi na kutekeleza ule muunganiko uliopo kati ya marehemu (Kanisa la wateswa), watakatifu
wa mbinguni (Kanisa la washindi) na kanisa la wapiganaji ndio sisi na hivi kwa pamoja
ni kanisa moja familia ya Mungu.
Fundisho tulilolisikia juu ya muunganiko wa
kanisa shindi, kanisa la wateswa na kanisa la mahujaji linawekwa mbele yetu na Papa
Paulo VI akisema “sisi twasadiki ushirika wa waamini wote wa Kristo, wa wale walio
bado safarini duniani, wa wale waliokufa ambao wanapata utakaso, wa wale wenye heri
ya mbingu, wote pamoja hufanya kanisa moja tu. Nasi twasadiki kwamba, katika umoja
huu, mapendo ya huruma ya Mungu na ya watakatifu wake yasikiliza daima sala zetu”
(KKK 962) Ndiyo kusema kuwaombea marehemu ni sehemu ya imani yetu, ni upendo kwa jirani
tukiitikia injili ya Bwana ya kumsaidia aliye katika taabu, aliyemhitaji.
Kuwaombea
marehemu ni kielelezo kimojawapo cha imani yetu katika ufufuko, kwa maana kama hatusadiki
yakuwa Kristu alikufa na kufufuka imani yetu ni bure. Ni kutokana na msingi huo twaamini
kwamba wale waliolala usingizi katika Yesu Kristu mfufuka, parapanda ya Mungu ikilia
watafufuliwa kwanza nasi tuliosalia tutanyakuliwa kwa kuwafuata wao.
Kuwaombea
marehemu ni jambo la thamani na la imani ambalo si la leo bali limekuwepo katika safari
ya wokovu. Tunasoma daima katika kitabu cha pili cha Wamakabayo kuwa Yuda kiongozi
wa Wayahudi alichanga fedha kwa kila mtu jumla drakma mbili elfu, akazipeleka Yerusalemu
kutoa sadaka ya dhambi. Kwa kufanya hivi alitenda vema na kwa haki kwa kuwa aliukumbuka
ufufuo wa wafu. Alifanya hili kwa sababu ya imani na kama asingekuwa na imani kuwa
wafu watafufuliwa ingekuwa upumbavu na kazi bure kuwaombea marehemu. (Rej. 2Wak. 12:
43-45).
Basi ndugu yangu mpendwa, ninakualika katika msingi uleule wa imani
katika ufufuko, kusali daima sala hii “raha ya milele uwape Ee Bwana na mwanga wa
milele uwaangazie wapumzike kwa amani, amina”. Ni Sala ya kujenga urafiki na marehemu
walioko toharani na hatimaye watakatifu wa mbinguni. Ni sala ambayo yatukumbusha wapendwa
wetu ambao wengine tuliwafahamu kwa karibu na hivi yatudai wajibu wa kuomba huruma
ya Mungu kwa ajili yao pasipo kukoma.
Mama Kanisa ametuwekea Misa tatu kwa
ajili ya marehemu wote ili kwa njia hiyo marehemu wapate msaada wa masitahili ya Kristo
kwa njia sadaka yake ya msalabani. Anataka asiwepo hata mmoja atakayekosa huruma na
msaada wa Mungu. Katika Misa hizi tatu injili zagusa Heri Nane njia ya utakatifu
na habari ya ufufuko wa wafu lililotumaini letu na imani yetu tunaposafiri kuelekea
ukamilifu yaani uzima wa milele ambao huja baada ya kifo. Tunasali na kutumaini kuwa,
kwa kifo maisha hayaondolewi ila hugeuzwa na kuwa maisha mapya, maisha makamilifu.
Basi
mpendwa mwanatafakari, leo ni wakati wa kusali na kuwatembelea waliolala kule makaburini
ili muunganiko katika sala ukamilishwe katika upendo unaoonekana katika maisha ya
watu. Yafaa pia kufunga kidogo kwa ajili ya wapendwa wetu ili kuisimika sala yetu
katika majitoleo ya Kristu mteswa na hatimaye uibuke na ushindi wa Kristo mfufuka.
Kumbukeni pia kujiombea wewe mwenyewe kwa maana kwakukumbusha kujitayarisha
kwa ajili ya safari ya kugeuzwa na kuingia maisha mapya, maisha ya mbinguni. Tumsifu
Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.