2013-10-31 09:36:50

Wizi wa shaba Reli ya Tazara wapatia dawa!


Jeshi la Polisi Nchini Tanzania kupitia Kikosi cha Polisi Tazara limefanikiwa kuutokomeza uhalifu na wizi wa shaba uliokuwa unafanyika katika reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) baada ya kuishirikisha jamii kwa kutumia dhana ya Polisi jamii na ulinzi shirikishi.

Hayo yalisemwa na Kamanda wa Kikosi cha Polisi TAZARA, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Rashid Seif wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Mkutano wa 39 Wakuu wa ulinzi na usalama kutoka mashirika ya reli na bandari kwa nchi za kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Kamanda Seif alisema kwa kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyopo katika maeneo ambayo reli ya Tazara inapita wamekuwa wakipata taarifa ambazo zimesababisha kuzuia matukio ya wizi wa shaba ambapo tangu mwezi April mpaka sasa hakuna tukio ambalo limetokea hali ambayo alisema imefanya watumiaji wa reli hiyo kuwa na imani ya kuendelea kusafirisha mizigo yao.

Aidha alisema Kikosi hicho kwa kushirikiana na uongozi wa Tazara wameweza kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa miundominu ya reli ambapo matukio ya uharibifu wa miundominu yamepungua kwa kiasi kikubwa na lengo ni kuhakikisha uhalifu unapungua kwa asilimia sabini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mkutano huo Bw. Neil Naidu kutoka Shirika la Reli la Transnet la Afrika kusini alisema malengo ya mkutano huo ni kubadilishana mbinu za kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka na uhalifu unaotokea mara kwa mara katika reli na bandari zilizopo katika nchi wanachama SADC.

Alisema katika kupambana na uhalifu huo ni lazima kufanya kazi kwa pamoja kwa kubadilishana taarifa za uhalifu na wahalifu pamoja na wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama wa bandari na reli ili kuhakikisha mizigo inayotumia njia hizo za usafiri inakuwa salama.

Alibainisha kuwa katika mkutano wao huo wa siku tatu watatoka na maazimio pamoja na mikakati itakayolenga kutokomeza wizi wa mizigo katika reli, bandari, uharibifu wa miundominu ya reli na makosa yanayovuka mipaka kwa kushirikiana na wadau wanaosafirisha mizigo kupitia bandari na reli kwa nchi wanachama wa SADC.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi za Botswana, Zambia, Tanzania, Swaziland na Afrika kusini ambapo mkutano wa mwisho ulifanyika nchini Zambia mwezi Aprili mwaka huu.








All the contents on this site are copyrighted ©.