2013-10-31 11:01:14

Vatican haina "Presha" na uvumi kuhusu upelelezi unaofanywa na Marekani!


Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anasema, Vatican haina muda wa kujihusisha na shutuma zilizotolewa na gazeti moja linalochapishwa nchini Italia kwamba, kati ya viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa ambao simu zao zilikuwa zinapelelezwa ni pamoja na viongozi wakuu kutoka Vatican.

Jarida la "Panorama" linadai kwamba, upelelezi huu umefanywa na Wakala wa Usalama wa Taifa Marekani kuanzia Desemba 2012 hadi tarehe 8 Januari 2013, hata wakati wa mkutano wa Makardinali kwa ajili ya kumchagua Papa mpya.

Padre Lombardi katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Padre Ciro Benedettini anasema kwamba, Vatican kimsingi haina taarifa zozote kuhusiana na viongozi wakuu wa Kanisa kufanyiwa upelelezi kwa njia ya simu na kwamba, hata kama jambo hilo limefanyika, Vatican haina wasi wasi wote kuhusiana na jambo hili. Baadhi ya viongozi wakuu wa Serikali Barani Ulaya wameonesha kusikitishwa kwao na taarifa kwamba, simu zao zilizkuwa zinadhibitiwa na Wakala wa Usalama wa Taifa nchini Marekani kwa malengo ya kisiasa, kiuchumi na kiulinzi.







All the contents on this site are copyrighted ©.