2013-10-31 11:28:19

Mshikamano wa Maaskofu kwa wananchi waliokumbwa na baa la njaa Kusini mwa Angola


Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa Mwaka uliokuwa unafanyika mjini Luanda. Maaskofu wamepembua na kutoa mikakati na mipango ya Kanisa Katoliki nchini Angola, Sao Tome na Principe kwa siku za usoni.

Maaskofu pamoja na mambo mengine wameangalia kwa kina na mapana kuhusu baa la njaa linalowakabili wananchi wengi wanaoishi Kusini mwa Angola. Maaskofu wanawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Angola kuonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa waathirika wa baa la njaa linalotishia usalama wa maisha ya mamillioni ya watu Kusini mwa Angola. Maaskofu wanatarajia kuanzisha Kampeni ya kuhamasisha mshikakano wa upendo na waathirika wa baa la njaa. Maaskofu wameguswa na maendeleo yanayojitokeza katika Manispaa na miji kadhaa nchini humo.

Kwa namna ya pekee, Maaskofu wamelaani kitendo cha kunajisi Sanamu ya Bikira kilichofanyika hivi karibuni kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Muxima. Taarifa inaonesha kwamba, watu sita ambao bado hawajatiwa mikononi mwa vyombo vya sheria, walifika Kanisani hapo na kuharibu Sanamu ya Bikira Maria na baadhi ya Sanamu zilizokuwepo Madhabahuni hapo.







All the contents on this site are copyrighted ©.