2013-10-31 09:28:05

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo Tanzania kwa Mwaka 2014- 2015


Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea Hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Mheshimiwa Stephen Masato Masira (MB), akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa Maendeleo wa taifa 2014/15 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likikaa kama Kamati ya mipango.

UTANGULIZI

    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likae kama Kamati ya Mipango ili liweze kupokea na kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15 ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12‐2015/16).


    Mheshimiwa Spika, awali ya yote, sina budi kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Mipango kwa maelekezo yake ambayo yametuwezesha kutekeleza majukumu ya usimamizi na uratibu wa miradi ya maendeleo. Aidha, napenda kutumia nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa kunipatia fursa ya kuwasilisha Mapendekezo haya. Vilevile, nitumie fursa hii kumshukuru Mhe. Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na Wajumbe wa Kamati kwa ushirikiano, maelekezo na ushauri. Tume ya Mipango itaendelea kuzingatia maoni na mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge katika uandaaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.



    Mheshimiwa Spika, napenda pia nitumie fursa hii kumshukuru Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. William Mgimwa (Mb) kwa ushirikiano wake wakati wa maandalizi ya mapendekezo haya. Aidha, nawashukuru Dkt. Philip Mpango, Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango pamoja na wataalam wake, na Dkt Servacius Likwelile, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha pamoja na wataalam wake kwa ushirikiano katika kufanikisha uandaaji wa Mapendekezo ninayowasilisha.


    Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15 ni ya nne katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Hivyo, Mapendekezo haya yamezingatia vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano vifuatavyo: (i) Miundombinu; (ii) Kilimo; (iii) Viwanda vinavyotumia malighafi za ndani na kuongeza thamani; (iv) Maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi; na (v) Uendelezaji wa huduma za utalii, biashara na fedha.


UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2012/13 NA ROBO YA KWANZA YA MWAKA 2013/14

    Mheshimiwa Spika, naomba nieleze kwa kifupi utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2012/13 hususan kwa maeneo ya kitaifa ya kimkakati. Kimsingi katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2012/13, mafanikio yamepatikana katika sekta mbali mbali licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa.


Mwenendo wa Uchumi kwa Mwaka 2013
    Mheshimiwa Spika, taarifa za awali zinaonesha kuwa Pato halisi la Taifa lilikua kwa kiwango cha asilimia 7.0 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2013 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Sekta zilizokuwa na viwango vikubwa vya ukuaji ni pamoja na usafiri na mawasiliano (18.4%), fedha (14.6) na ujenzi (8.7%). Katika kipindi cha miezi tisa (9) iliyopita kasi ya mfumuko wa bei imekuwa ikiendelea kupungua kutoka asilimia 10.9 Januari, 2013 hadi asilimia 6.1 Septemba, 2013. Kupungua kwa kasi ya upandaji bei kumetokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula hususan mpunga, mahindi na mtama.


    Mheshimiwa Spika, hali ya mwenendo wa uchumi wa Dunia sio ya kuridhisha kutokana na kupungua kwa mahitaji na ongezeko dogo la ukuaji wa uchumi kwa Nchi Zinazoibukia Kiuchumi; kudhoofika kwa shughuli za kiuchumi na biashara ya kifedha katika nchi za Ulaya kulikosababishwa na mgogoro wa madeni (Euro Debt Crisis); na kupungua kwa kiwango cha ukuaji kwa nchi ya Marekani. Kulingana na Taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF ya Julai 2013, Pato la Dunia linatarajiwa kukua kwa asilimia 3.1 mwaka 2013 sawa na ilivyokuwa katika mwaka 2012.


    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ukuaji wa Pato unaonesha kuanza kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2013 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2012. Ukuaji kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki nao unaonesha kuimarika kwa nchi zote wanachama kwa kuwa na viwango vinavyoongezeka isipokuwa kwa nchi ya Rwanda. Kasi ya ukuaji wa uchumi kwa nchi hizo kwa mwaka 2012 ikilinganishwa na mwaka 2013 inatarajiwa kuongezeka kama ifuatavyo: Tanzania kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 7.0; Kenya kutoka asilimia 4.7 hadi 5.9; Uganda kutoka asilimia 2.6 hadi asilimia 4.8; na Burundi kutoka asilimia 4.0 hadi asilimia 4.5. Kwa Upande wa Rwanda, kasi ya ukuaji inatarajiwa kupungua kidogo kutoka asilimia 7.7 mwaka 2012 hadi asilimia 7.6 mwaka 2013.


    Mheshimiwa Spika, Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2012 ilionesha idadi ya watu Tanzania Bara ilikuwa milioni 43.6 ikilinganishwa na makadirio ya idadi ya watu milioni 43.2 mwaka 2011. Hivyo, pato la wastani la kila mtu liliongezeka kwa asilimia 17.9 na kuwa dola za kimarekani 647 sawa na shilingi 1,025,038 mwaka 2012 ikilinganishwa na dola za Kimarekani 550 sawa na shilingi 869,436.3 mwaka 2011. Aidha, idadi ya watu Tanzania inatarajiwa kufikia milioni 63 na kulingana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Pato la wastani la kila mtu linatakiwa liwe limefikia dola za Kimarekani 3,000 sawa na shilingi 4,836,000 ifikapo mwaka 2025. Hivyo, ili kufikia pato hilo la wastani kwa kila mtu na kufikia hadhi ya nchi ya kipato cha kati (dola za Kimarekani 1,036 hadi 4,085) sawa na takriban shilingi 1,670,032 hadi 6,586,632, ni dhahiri tunahitaji msukumo mkubwa katika ukuaji wa sekta zote hususan sekta ya kilimo yenye kuajiri watu wengi.



Mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2012/13

    Mheshimiwa Spika, sasa naomba nieleze kwa kifupi hali ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2012/13 na robo ya kwanza ya mwaka 2013/14 kwa baadhi ya miradi ya maendeleo.


    Mheshimiwa Spika, katika eneo la reli, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kutandikwa kwa reli yenye urefu wa kilomita 42 na kufikisha jumla ya kilomita 136 zilizotandikwa ikilinganishwa na kilomita 197 za reli yenye uzito wa ratili 80 kwa yadi zilizokusudiwa katika reli ya kati; kuendelea kwa ujenzi wa madaraja matatu ya reli, mawili kati ya Kilosa na Gulwe na moja kati ya Bahi na Kintinku; kukamilika kwa matengenezo katika maeneo 13 kati ya stesheni ya Godegode na Gulwe na maeneo 32 yaliyopo kati ya stesheni za Kilosa na Gulwe; na kufanya malipo ya awali kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa 34 ya breki, mabehewa 22 ya abiria na injini mpya 13 kwa ajili ya reli ya kati. Aidha matayarisho ya kuijenga upya reli ya kati yanaendelea ambapo upembuzi yakinifu umekamilika. Serikali ipo katika hatua ya kukamilisha upembuzi wa kina na imeanza kumtafuta mwekezeji wa kujenga upya reli hiyo.


    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa reli ya Kikanda, hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa reli ya Dar es Salaam – Isaka – Kigali - Keza - Msongati (km 1,464) ni kuendelea na kazi ya kukamilisha taarifa ya mwisho ya upembuzi wa kina inayofanywa na Mshauri Mwelekezi Kampuni ya CANARAIL kutoka Canada. Aidha, kuhusu reli ya Tanga – Arusha - Musoma, hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa ulipaji wa fidia kwa wakazi wa eneo la Mwambani (Tanga) ili kupisha ujenzi wa sehemu ya kupanga mabehewa; na kukamilika kwa taratibu za kumpata mtaalam mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa reli.


    Mheshimiwa Spika, katika kuboresha usafiri wa reli jijini Dar es Salaam, kazi zilizofanyika katika mwaka 2012/13 ni: kukarabati, kuimarisha na kupanua tuta la njia ya reli kati ya eneo la Mnyamani na Mwananchi; kufanya matengenezo ya makutano ya njia ya reli na barabara pamoja na kuweka alama za usalama; ujenzi wa sehemu za kupandia na kushukia abiria; ujenzi wa sehemu za kupishania treni; na kujenga vizuizi vya magari sehemu ambazo treni inakatisha barabara.


    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa barabara, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: ujenzi wa kilomita 558.92 za barabara kuu kwa kiwango cha lami ikilinganishwa na lengo la kilomita 414; na ukarabati wa kilomita 257.53 wa barabara kuu kwa kiwango cha lami umekamilika ikilinganishwa na lengo la kukarabati kilomita 135.


    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa madaraja, mafanikio ni pamoja na: kukamilika kwa ujenzi wa madaraja ya Ruhekei (Mbinga) na Nanganga (Tunduru); na kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Nangoo (Mtwara), Maligisu (Mwanza), Malagarasi (Kigoma), na Mbutu (Igunga) ambao upo katika hatua za mwisho kukamilika. Kwa upande wa daraja la Kigamboni, daraja la muda limekamilika na kazi za ujenzi wa daraja imeanza ambapo nguzo 150 kati ya 202 zimekamilika na kusafishwa kwa eneo la barabara zinazoingia katika daraja. Kuhusu vivuko, kazi zilizofanyika ni pamoja na: kukamilika kwa ukarabati wa kivuko cha MV Chato (Kagera) na ununuzi wa kivuko kipya cha Ilagala (Kigoma).



    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa bandari mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa gati nambari 1 hadi 7 katika bandari ya Dar es Salaam; kukamilika kwa upembuzi yakinifu na kusainiwa kwa makubaliano ya awali kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Watu wa China kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Mbegani (Bagamoyo); kukamilika kwa upembuzi yakinifu na kutangaza mradi wa bandari ya Mwambani (Tanga) ili kupata wawekezaji wa kuendeleza bandari kwa ubia. Kuhusu bandari kavu Kisarawe, hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa mchakato wa zabuni kwa ajili ya upembuzi yakinifu awamu ya pili na Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe kukamilisha taratibu za kupata kibali kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi cha kutenga eneo la ekari 1,760 badala ya ekari 1,468 za awali.


    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa miradi ya maji safi na majitaka, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kusimikwa kwa mitambo ya umeme na mashine za kusukuma na kusafisha maji katika mradi wa Ruvu Chini na kutandazwa kwa mabomba katika eneo la kilomita 17.1 kati ya kilomita 55 zilizokusudiwa. Kwa upande wa mradi wa maji Ruvu Juu, ripoti ya usanifu kwa ajili ya kutandaza bomba kuu kutoka mtamboni hadi Kibamba, na ujenzi wa tanki jipya eneo la Kibamba, umekamilika Novemba, 2012 na kukamilika kwa taratibu za kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi, Agosti, 2013. Aidha, idadi ya wakazi wa vijijini wanaopata maji safi imeongezeka kutoka watumiaji milioni 20.6 mwaka 2011 hadi milioni 22.29 mwaka 2012.


    Mheshimiwa Spika, katika eneo la nishati, kazi zilizofanyika katika mradi wa Bomba la Gesi (Mtwara - Dar es Salaam) ni: kukamilika kwa ulipaji wa fidia ya jumla ya shilingi bilioni 6.86 kwa wananchi, kupatikana kwa cheti cha mazingira tangu mwezi Aprili 2012, kuwasili kwa mabomba ya gesi 20,491 yenye uwezo wa kujenga kilomita 243.86 na kutandazwa kwa mabomba yenye urefu wa kilomita 108 ambapo mabomba yenye urefu wa kilomita 25.8 yameunganishwa.


    Mheshimiwa Spika, katika mradi wa mtambo wa kufua umeme Kinyerezi I (MW 150) hatua iliyofikiwa ni kuingia mkataba kati ya Serikali na Mkandarasi (M/s Jacobsen Electro AS) kutoka Norway na mshauri wa mradi (M/s Lahmeyer) kutoka Ujerumani. Mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuboreshwa kwa miundombinu ya usambazaji wa umeme jijini Dar es Salaam katika vituo vya Buguruni, katikati ya jiji, Kariakoo, Kipawa, Mbagala, Mbezi, Oysterbay na Ubungo kwa kufungwa kwa transfoma zenye uwezo wa MVA 15 kwa kila kituo.


    Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika miradi ya umeme vijijini ni pamoja na: kupeleka umeme Makao Makuu ya Wilaya za Namtumbo, Nyang’hwale na Nkasi; kupata Mkandarasi wa kupeleka umeme makao makuu ya wilaya za Bukombe na Mbogwe; kukamilisha tathmini ya zabuni za kuwapata wakandarasi wa kutekeleza Awamu ya Pili ya Mpango Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini; kukamilisha ujenzi wa kilomita 24.78 kati ya 47.53 za njia za usambazaji umeme na kufunga transfoma 7 kati ya 24 mkoani Mtwara na kuunganisha umeme kwa wateja 277; na kukamilisha ujenzi wa jumla ya kilomita 11.28 kati ya 28.20 za njia ya umeme ya msongo wa kV 33 na kV 11 katika mkoa wa Lindi. Aidha, ujenzi wa kilomita 59.5 kati ya 72.3 za njia ya umeme ya msongo wa kV 0.4 mkoani Lindi umekamilika na transfoma 5 kati ya 25 zimefungwa, na wateja 132 wameunganishiwa umeme.


    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kilimo, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kutambua na kuhakiki mashamba yenye ukubwa hekta 334,538 kwa ajili ya uwekezaji katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Rufiji, Kagera, Kilombero na Malagarasi ambapo hekta 85,000 zimepata hatimiliki. Aidha, kazi ya kupima maeneo inaendelea katika bonde la Rufiji - Mkongo Block ambapo jumla ya hekta 5,551 zimepimwa. Kwa upande wa miradi ya Ukanda wa SAGCOT, hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa asilimia 40 ya ujenzi wa banio katika mradi wa umwagiliaji – Itete, Morogoro (Hekta 1,000). Aidha, katika miradi ya umwagiliaji ya Mpanga –Ngalimila, Morogoro (Hekta 31,500), Sonjo – Kilombero (Hekta 1,340) na Lupilo, Morogoro (Hekta 4,000), kazi ya upembuzi yakinifu imekamilika na kazi za usanifu na kuandaa michoro ya skimu inaendelea.



    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula, ujenzi wa ghala katika kanda ya Songea lenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 upo katika hatua za mwisho. Aidha, michoro kwa ajili ya ujenzi wa ghala la Mbozi na ghala jingine Songea imekamilika. Vile vile, majadiliano kati ya Serikali na benki ya Exim ya China yameanza kwa ajili ya kupata mkopo wa kujenga vihenge vya kisasa (silos) vyenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya tani 160,000 katika kanda za Kipawa, Makambako, Sumbawanga, Songea, Shinyanga, Arusha na Dodoma.



    Mheshimiwa Spika, Katika sekta ya viwanda, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilisha uchorongaji wa mashimo 40 yenye jumla ya urefu wa mita 8,000 kwa ajili ya kuhakiki wingi wa chuma katika eneo la Liganga; na kukamilisha tathmini ya eneo la Kurasini ekari 60 lenye thamani ya shilingi bilioni 94.1 Mei, 2013 na kulipa fidia ekari 19.6 kwa kaya 278. Aidha, ulipaji fidia ya kiasi cha shillingi bilioni 16.9 kwa eneo la Bagamoyo ulifanyika mwaka 2011/12 na mwaka 2012/13 kwa hekta 1,600 kati ya 5,700 zilizofanyiwa tathmini ya shillingi bilioni 58.8 mwaka 2011. Kwa upande wa Kigoma, malipo ya shilingi bilioni 1.5 kwa hekta 3,000 kati ya hekta 20,000 yalifanyika mwaka 2011/12. Mchakato wa kupata fedha za kumalizia kulipa fidia katika eneo la mradi Bagamoyo na Kigoma unaendelea kwa mwaka 2013/14.


    Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa kiwanda cha Viuadudu Kibaha, hatua iliyofikiwa ni ujenzi wa majengo mawili ya kiwanda; usanifu wa kina na kuanza ufungaji wa mitambo. Kiwanda hiki tayari kimezinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Oktoba, 2013. Kwa upande wa mradi wa Magadi Soda- Bonde la Engaruka (Arusha), kazi ya kuchoronga mashimo 12 kwa ajili ya kuhakiki wingi na ubora wa magadi imekamilika, ambapo imebainika kuwa eneo la Engaruka lina magadi yenye mita za ujazo bilioni 4.68 kiasi ambacho ni kikubwa kutosheleza uchimbaji magadi soda kwa zaidi ya miaka 400. Upatikanaji wa magadi soda utasaidia katika viwanda vya madawa, sabuni, nguo, rangi, na viwanda vya kuchakata chuma. Kwa sasa Serikali inaendelea na tafiti za kubaini tabia za ndege aina ya Flamingo ili kuendana na matakwa ya kimazingira, ujenzi wa miundombinu na kutafiti teknolojia bora za uchimbaji wa magadi soda.


    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa rasilimali watu, mafanikio yaliyopatikana hadi Juni, 2013 ni pamoja na: wataalamu wapatao 374 wameendelea kugharimiwa na Serikali katika nyanja maalum za gesi, mafuta, chuma, urani na madini mengine, na nyanja nyingine muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Kati ya hao, 261 ni wa shahada ya uzamili na 133, shahada ya uzamivu na wanasoma katika vyuo vikuu sita vya umma ambavyo ni Dar-es Salaam, Sokoine, Muhimbili, Mzumbe, Ardhi na Nelson Mandela.


    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kugharamia miradi ya utafiti hapa nchini ikiwa ni pamoja na ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya utafiti, kutengeneza mitambo na vipuri. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilisha ukarabati wa matrekta 11 kati ya 14 ambao umefanywa na CAMARTEC; kukamilika kwa matengenezo ya vipuri vya treni, reli, na trekta ndogo za mikono (power tiller) yaliyofanywa na Taasisi ya Tanzania Automotive Technology Centre (TATC) iliyopo Kibaha; na kuendeleza ubunifu na uendelezaji wa mashine mbalimbali kwa ajili ya usindikaji mazao.


    Mheshimiwa Spika, katika eneo la huduma za fedha, mafanikio yaliyopatikana ni kuundwa kwa bodi ya wakurugenzi, na kuanza kuajiri maafisa waandamizi na kuongeza mtaji wa Benki ya Kilimo kufikia shilingi bilioni 90; kuongeza mtaji wa shilingi bilioni 50 kwa Benki ya Rasilimali Tanzania na kufikia shilingi bilioni 142; na kuongeza mtaji wa shilingi bilioni 1.1 kwa Benki ya Wanawake Tanzania na kufikia shilingi bilioni 8.2.


    Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu malengo na hatua ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2012/13 na robo ya kwanza kwa mwaka 2013/14 kwa baadhi ya maeneo yakijumuisha mafanikio yaliyopatikana kwa upande wa sekta binafsi yapo katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15 (Sura ya pili).


Changamoto na Hatua Zilizochukuliwa

    Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2012/13, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, kumekuwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na:- ufinyu wa rasilimali fedha hususan upatikanaji wa mikopo ya kugharamia miradi; taratibu za tathmini ya fidia na ulipaji fidia kwa wakati; upatikanaji wa ardhi iliyopimwa kwa ajili ya uwekezaji; upatikanaji wa huduma wezeshi hususan barabara, maji na umeme katika maeneo ya miradi; na madeni ya miaka iliyopita kwa baadhi ya miradi.


    Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na: kuendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato; kuandaa mwongozo wa andiko la miradi kwa ajili ya kuziwezesha wizara kuandaa miradi itakayokidhi vigezo vya mikopo; kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi chini ya President’s Delivery Bureau; na kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

MAENEO MUHIMU YA MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2014/15

    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Serikali itaendelea kuelekeza fedha za maendeleo kwenye miradi michache ya kitaifa ya kimkakati na yenye kuleta matokeo makubwa ili kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi, na hivyo kuongeza ajira, uzalishaji hususan katika sekta ya kilimo kwa lengo la kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei, kuimarisha ushindani wa kiuchumi, kuongeza mauzo nje ya nchi na kupunguza umasikini.


    Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia fursa za kikanda na dunia, jitihada za ziada zinahitajika ili kuhakikisha kuwa zinaleta matokeo chanya na kwa haraka. Hivyo, inapendekezwa kuwa masuala muhimu yafuatayo yazingatiwe katika kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15:


    Kudumisha amani na utawala bora kama msingi muhimu wa kuwezesha uzalishaji mali, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii;
    Ukuaji uchumi unakuwa shirikishi ili kuondoa tofauti za kipato na kupunguza umaskini;
    Kuongeza tija katika kilimo hususan mazao yenye thamani kubwa (high value crops);
    Ubunifu na maendeleo ya teknolojia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii;
    Masoko kwa bidhaa za ndani na vyanzo vipya vya uwekezaji katika uchumi wa Kikanda na Dunia vinatumika vizuri;
    Kujenga uwezo wa kuhimili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi;
    Kujenga uwezo wa kutumia vizuri mapato yatakayotokana na gesi asilia na madini mengine yanayoendelea kugunduliwa;
    Kutumia fursa ya ongezeko la watu nchini kuleta manufaa ya kiuchumi (Demographic Dividend), kwa kupunguza kiwango cha utegemezi, yaani uwiano kati ya watoto ambao ni tegemezi na idadi ya watu wanaofanya kazi; na
    Kutumia fursa ya ongezeko kubwa la watu mijini kwa kuifanya miji kuwa vituo endelevu vya ubunifu na ukuaji uchumi.

Maeneo ya Kipaumbele kwa Mwaka 2014/15

    Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia masuala muhimu niliyoainisha, sasa naomba nielezee kwa kifupi maeneo ya kitaifa ya kimkakati ya kipaumbele katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2014/15. Maeneo ya kipaumbele yanajumuisha miradi iliyoibuliwa katika progamu ya Matokeo Makubwa Sasa ambayo yapo katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15, kiambatisho A.


    Maeneo ya Kitaifa ya Kimkakati na Programu ya Matokeo Makubwa Sasa


    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Miundombinu, maeneo yatakayopewa kipaumbele ni:


    Nishati: kuendelea kutekeleza miradi iliyoibuliwa chini ya programu ya Matokeo Makubwa Sasa ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa bomba la Gesi kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam; na kuendelea kuboresha miundombinu ya ufuaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme mijini na vijijini. Aidha, Serikali itaendelea na uwekezaji katika vyanzo vingine vya nishati mbadala, jadidifu na makaa ya mawe; na kuweka mazingira wezeshi ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali za gesi asilia.
    Barabara: kutekeleza miradi ya barabara iliyoibuliwa katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa hususan ujenzi na ukarabati wa barabara zinazofungua maeneo yenye fursa za kiuchumi; na kuboresha na kusimamia viwango vya usalama barabarani.
    Reli: Serikali itaendelea kuimarisha reli ya kati hususan miradi iliyoibuliwa katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa ikiwa ni pamoja ukarabati wa miundombinu ya reli ikijumuisha majengo ya stesheni na madaraja; kuanzisha mpango wa biashara (business plan) na mfumo wa madhubuti wa ufuatiliaji wa mizigo; na ukarabati na ununuzi wa injini na mabehewa ya treni kwa ajili ya reli ya kati. Maeneo mengine ni kuendelea kukamilisha upembuzi wa kina na kumpata mwekezaji wa kujenga upya reli ya kati kwa kiwango cha geji ya kisasa; kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, na kutafuta wawekezaji katika miradi mipya ya reli; kuboresha usafiri wa reli jijini Dar es Salaam na kuendelea kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa reli.
    Bandari: kujenga na kuboresha miundombinu ya bandari iliyoanishwa kwenye Programu ya Matokeo Makubwa Sasa hususan kuboresha mfumo wa mawasiliano katika bandari ya Dar es Salaam; na kuboresha miundombinu ya reli iliyopo bandarini. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa bandari.
    Usafiri wa Anga: kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuongeza ufanisi; na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege katika maeneo ya kimkakati.
    Maji Safi na Majitaka: kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika Progamu ya Matokeo Makubwa Sasa hususan kuimarisha na kuongeza miundombinu ya maji vijijini ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi na majitaka katika Jiji la Dar-es Salaam na miji mingine nchini kwa kuboresha, kukarabati na kuongeza miundombinu na vyanzo vipya.
    Teknolojia ya Habari na Mawasiliano: kuendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; kuanzisha maeneo maalum ya TEHAMA; utekelezaji wa mradi wa Anuani za Makazi na Misimbo ya Posta; na kuhamasisha na kukuza tafiti za kimaendeleo.


    Mheshimiwa Spika, katika sekta ya Kilimo, maeneo yatakayopewa kipaumbele ni:- kuendeleza miradi ya kilimo katika programu ya Matokeo Makubwa Sasa ikiwa ni pamoja na kuendeleza kilimo cha kisasa kwenye skimu za wakulima wadogo wa mpunga; kutafuta mashamba kwa ajili ya wawekezaji wakubwa; na kuanzisha mfumo wa maghala ya masoko ya mazao (collective warehouse based marketing system). Maeneo mengine ni: utekelezaji wa miradi ya miwa na mpunga katika maeneo ya mabonde ya Wami, Ruvu, Kagera, Kilombero na Malagarasi; utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji katika ukanda wa SAGCOT; kujenga na kukarabati miundombinu ya umwagiliaji, kuimarisha vituo vya tafiti za kilimo; kuwezesha na kuimarisha Ushirika nchini; na kuendelea na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula.


    Mheshimiwa Spika, katika sekta ya Mifugo, maeneo yatakayopewa kipaumbele ni: kuendeleza na kuboresha miundombinu ya mifugo kama vile malisho, majosho, na malambo; kujenga na kuimarisha vituo vya uhamilishaji; kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na kuimarisha vituo vya tafiti za mifugo. Kwa upande wa sekta ya Uvuvi, maeneo ya kipaumbele ni: kuimarisha usimamizi wa uvuvi katika eneo la Bahari Kuu ili kuongeza mapato; kuimarisha zana za ukaguzi na uvunaji wa samaki; kukuza huduma na miundombinu ya uzalishaji wa samaki na kuimarisha vituo vya tafiti za uvuvi.


    Mheshimiwa Spika, katika sekta ya Viwanda, maeneo ya kipaumbele ni: kuendelea kutambua na kutenga maeneo ya ardhi ya uwekezaji, hususan katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZ/SEZ); ujenzi wa Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini; kuongeza kasi ya kuvutia wawekezaji na kujenga mazingira wezeshi katika sekta ya viwanda; kujenga miundombinu muhimu katika kuendeleza mradi wa chuma - Liganga na mradi wa magadi soda katika bonde la Engaruka; kuendeleza miradi ya kukuza ajira kwa vijana kwa kuimarisha viwanda vidogo chini ya SIDO; kukuza maendeleo ya wajasiriamali wadogo na wa kati kwa kuanzisha maeneo maalum ya viwanda na uhaulishaji wa teknolojia ya uzalishaji wa matrekta na zana za kilimo.


    Mheshimiwa Spika, katika Maendeleo ya Rasilimali Watu, maeneo ya kipaumbele ni: kuendelea na utekelezaji wa miradi ya elimu katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa hususan mpango wa kuwezesha wanafunzi na walimu kujifunza kwa shule za msingi na sekondari; kuimarisha mfumo wa ruzuku ya kuendesha shule; na ujenzi wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia. Maeneo mengine ni: kuendelea kutoa mafunzo katika nyanja maalum hususan katika gesi na mafuta, chuma, urani, madini, umwagiliaji na maji; na kuendeleza elimu ya ufundi stadi kwa kuongeza na kuboresha miundombinu na mitaala katika vyuo vya ufundi na vyuo vya maendeleo ya jamii; upanuzi wa vyuo vya ualimu hasa katika masomo ya sayansi na vituo vya utafiti; na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu.


    Mheshimiwa Spika, katika sekta ya Huduma za Fedha na Utalii, maeneo ya kipaumbele ni: kuongeza mitaji na matawi katika Benki ya Kilimo, Benki ya Rasilimali na Benki ya Wanawake; kujenga uwezo wa utoaji huduma na mikopo; na mafunzo kwa wajasiriamali. Aidha, Serikali itaendelea kupanga na kutangaza utalii; na kushirikisha sekta binafsi kuwekeza zaidi katika maeneo yenye vivutio vya utalii.


    Maeneo mengine Muhimu kwa ukuaji wa Uchumi


    Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo kwa maeneo ya Kitaifa ya kimkakati na Programu ya Matokeo Makubwa Sasa, kutahitajika uwekezaji katika maeneo mengine ambayo yana uhusiano na maeneo ya kipaumbele ya kitaifa. Miradi katika maeneo haya, itaibuliwa na sekta/mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na sekta binafsi na kutekelezwa katika ngazi mbalimbali.


    Mheshimiwa Spika, maeneo yatakayozingatiwa ni: Elimu/Mafunzo ya Ufundi, Madini, Mifugo na Uvuvi, Misitu na Wanyamapoli, Afya na Ustawi wa Jamii, na Ardhi Nyumba na Makazi. Maeneo mengine ni Usafiri wa Anga, Hali ya Hewa, Biashara na Masoko, Utawala Bora, Ushirikiano wa Kikanda, Utambulisho wa Taifa, Sensa ya Watu na Makazi, Katiba Mpya, Ajira na Mazingira.


    Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2014/15 yapo katika Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2014/15 (Sura ya tatu).



UGHARAMIAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2014/15

    Mheshimiwa Spika, Makadirio ya mahitaji ya rasilimali fedha ya kugharamia bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/15 ni shilingi bilioni 19,909.7. Kati ya hizo, shilingi bilioni 11,713.6 zitatokana na mapato ya ndani, shilingi bilioni 1,148.0 ni mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara, shilingi bilioni 2,898.2 ni mikopo ya ndani na shilingi bilioni 3,772.0 ni misaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo. Kiasi hicho cha fedha kitagharamia matumizi ya kawaida ya shilingi bilioni 14,642.4 na miradi ya maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 5,267.3 sawa na asilimia 26.45 ya bajeti ya Serikali. Kati ya bajeti ya maendeleo, fedha za ndani ni kiasi cha shilingi bilioni 2,643.3 na kiasi cha shilingi bilioni 2,624.0 ni fedha za nje.


    Mheshimiwa Spika, izingatiwe kwamba, kiwango cha bajeti ya maendeleo hakikujumuisha fedha kwa ajili ya mfuko wa barabara na maendeleo ya rasilimali watu ambazo kwa mfumo wa sasa wa bajeti zinapangwa kama sehemu ya matumizi ya kawaida japokuwa kiuhalisia ni matumizi ya maendeleo. Kama vipengele hivyo vikijimuishwa, bajeti ya maendeleo inafikia takriban asilimia 31 ya bajeti yote.


    Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujikita katika kuwezesha sekta binafsi kuchangia katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kipaumbele itakuwa ni kutumia rasilimali chache kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi pamoja na kuendelea kuboresha mazingira ya kibiashara na uwekezaji ili kuvutia uwekezaji katika maeneo ya kipaumbele na yenye kuleta matokeo makubwa. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan, miradi ya miundombinu.

MAJUKUMU YA UTEKELEZAJI
    Mheshimiwa Spika, mara baada ya Mapendekezo haya kuridhiwa na Bunge, Wizara, Idara Zinazojitegemea na Wakala za Serikali zitatakiwa kuandaa na kuwasilisha Tume ya Mipango na Wizara ya Fedha miradi itakayotekelezwa katika sekta zao kwa mwaka 2014/15 wiki ya nne ya Januari 2014. Tume ya Mipango itafanya uchambuzi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na wizara za kisekta na miradi itakayopitishwa itajumuishwa katika kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15 na kitabu cha Bajeti ya Maendeleo 2014/15 (Vol 4). Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitatakiwa kuainisha miradi ya maendeleo na kuwasilisha mapendekezo ya miradi hiyo Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na Wizara ya Fedha kwa ajili ya kujumuishwa katika kitabu cha Bajeti ya Maendeleo (Vol 4).


HITIMISHO
    Mheshimiwa Spika, naomba sasa Bunge lako Tukufu likae kama kamati ya Mipango na kujadili mapendekezo niliyowasilisha, ili Serikali iweze kunufaika na ushauri na maoni ya Waheshimiwa Wabunge. Baada ya kupata maoni ya Wabunge, Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15 utaandaliwa na kuwasilishwa rasmi Bungeni mwezi Juni, 2014. Serikali itazingatia maoni na ushauri wa Kamati ya Mipango ya Bunge zima na kuyafanyia kazi ipasavyo.


    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.









All the contents on this site are copyrighted ©.