2013-10-31 14:15:59

Makardinali wapya kutangazwa Mwezi Februari 2014


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kufanya mkutano na Makardinali mapema mwezi Oktoba na baadaye kukutana na Baraza la Sinodi za Maaskofu, Baba Mtakatifu alionesha nia yake kwa wajumbe ya kutaka kuwatangaza Makardinali wapya, wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, hapo tarehe 22 Februari 2014.

Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine ameamua kwamba, kutafanyika mkutano wa Makardinali kutoka sehemu mbali mbali za dunia hapo Mwezi Februari 2014. Hayo yamefafanuliwa kwa kina na Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican.

Anasema kwamba, Baba Mtakatifu anapenda kuendeleza mapokeo kutoka kwa watangulizi wake kuhusu mikutano ya Makardinali. Baba Mtakatifu atapata fursa kwanza kabisa kukutana na Kikundi cha Makardinali wanane aliowateuwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kumpatia ushauri kama ilivyokuwa imependekezwa kwenye mikutano ya Makardinali.

Mkutano huu unatarajiwa kufanyika hapo tarehe 17 hadi tarehe 18 Februari 2014. Baada ya Mkutano wa Makardinali, kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 25 Februari 2014 kutafanyika Mkutano wa Baraza la Sinodi. Padre Lombardi anasema, Mwezi Februari, 2014, Baba Mtakatifu atakuwa na mikutano kadhaa kuhusu maisha na utume wa Kanisa, mikutano inayotarajiwa kuwahusisha Makardinali wengi zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.