2013-10-30 15:10:27

Papa Francisko asema, Matumaini ni zawadi itokayo kwa Roho Mtakatifu


Mapema Jumanne Baba Mtakatifu Francisko , akiongoza Ibada ya Misa katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta, Vatican, alihimiza Wakristu kuwa na tumaini thabiti kwa Kristu, kwa kuwa tumaini ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu.
Papa alielezea maana ya kweli ya tumaini akisema kwamba, tumaini la Mkristu ni zaidi ya matumiani ya kawaida, kwa kuwa, kutumaini katika Kristu ni kutarajia zawadi itokayo kwa Roho Mtakatifu , ni fumbo jipya ambalo kamwe halimtelekezi mtu.

Baba Mtakatifu Francisko alieleza kwa kurejea maneno ya Mtakatifu Paulo yanayosema, kumtumaini Kristu ni kuwa na tumaini lisilofadhaisha, au kutelekeza, kwa sababu ni zawadi itokayo kwa Roho Mtakatifu. Mtakatifu Paulo anaendelea kutuambia kwamba tumaini hili lina jina nalo ni Kristo.

Papa aliendelea kufafanua maana ya matumaini, akisema hujenga aina ya mvuto unaoelekea katika ufunuo wa Yesu Kristo , unao elekea katika furaha ya kweli ambayo ni uzima wa milele .


Na akirejea fadhila ya imani, matumaini na mapendo , Papa alisema kuwa mara nyingi fadhila ya matumaini ni unyenyekevu zaidi katika mambo haya tatu , kwa sababu , tumaini limefichika katika siri ya maisha. Mtakatifu Paulo anasema : ni motomoto wa fadhila katika matumaini ya Ufunuo, na wala si jambo la kufikirika.

Papa aliendelea kufundisha kwamba, Yesu, Tumaini la Mkristu, hubadilisha yote katika maisha. Hivyo matumaini yanakuwa ni muujiza wa mara kwa mara. Muujiza katika kile anachokifanya Yeye katika Kanisa lake, muujiza wa kufanya yote kuwa mapya. Na ni hivyo ndivyo, anavyo fanya katika maisha yangu, katika maisha yako na katika maisha yetu wote. Yeye hujenga na kukarabati. Na hutenda kwa haki kwa kuwa yeye ni tumaini la kweli. Kristo, ni Yeye anaye badilisha kila kitu katika maajabu ya Uumbaji. Ni Yeye kwa sababu ndiye tumaini letu, lisilo jishaua kwa sababu Yeye ni mwaminifu, na hawezi kujikana mwenyewe. Na hivyo Yeye ni fadhila na tumaini letu la kweli.

Na alihitimisha kwa kuwakumbusha Wakristo wote, kumgeukia Mama Bikira Maria , ambaye alibaki na tumaini hata wakati wa giza la kifo cha mwanae Msalabani hadi kufufuka kwake . Ni tumaini lililojaa ndani ya moyo wake lililomfariji wakati wa giza hicho katika maisha yake.lakini matumaini yalifanya upya kila kitu.
Papa alieleza na kutolea ombi kwa Mwenyezi Mungu, ili tupate neema hii ya moyo wa matumaini siku zote.








All the contents on this site are copyrighted ©.