2013-10-30 11:03:42

Marehemu Askofu Raymond Mwanyika, atakumbukwa na wengi!


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Jumanne tarehe 29 Oktoba 2013 ameongoza Familia ya Mungu nchini Tanzania katika mazishi ya Askofu mstaafu Raymond Mwanyika aliyefariki dunia hivi karibuni na kuzikwa kwenye Kanisa kuu la Jimbo Katoliki Njombe.

Askofu Ngalalekumtwa katika mahubiri yake amesema kwamba, Marehemu Askofu Mwanyika atakumbukwa na wengi kutokana na bidii, ari na moyo wake wa shughuli za kichungaji na maendeleo kwa wananchi wa Njombe katika ujumla wao. Ni muasisi wa Jimbo Katoliki la Njombe, aliyeshiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo endelevu kwa Kanisa na Jamii kwa ujumla. Alianzisha na kuimarisha Parokia kwa ajili ya kusogeza huduma za kichungaji kwa waamini wake.

Marehemu Askofu Mwanyika, alitamani kuona maendeleo ya mtu mzima, ndiyo maana alijitaabisha kuanzisha shule kwa ajili ya elimu, lakini alikazia majiundo makini ya wahudumu wa Injili kwa kuanzisha Seminari ndogo ya Kilocha. Aliwajengea vijana uwezo wa kujiajiri kwa kuanzisha vyuo vya ufundi stadi. Mikakati hii yote ni ushuhuda makini kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Njombe, waliokusanyika kwa wingi kumsindikiza Marehemu Askofu Raymond Mwanyika katika safari yake ya mwisho hapa duniani. Ibada hii imehudhuriwa na waamini, viongozi wa Makanisa, dini na Serikali.

Akitoa salam za rambi rambi kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Mohamed Gharib Bilal, amemshukuru na kumpongeza Marehemu Askofu Raymond Mwanyika kwa mchango wake kwa ajili ya maendeleo endelevu kwa wananchi wa Njombe. Alikuwa ni kiongozi aliyesimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na utulivu, changamoto kwa viongozi wa dini na Serikali nchini Tanzania kuendelea kuenzi misingi hii kwa ajili ya mafao ya wengi. Alishirikiana na Serikali pamoja na wadau mbali mbali katika kupanga na kutekeleza mikakati ya maendeleo kwa watu wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.