Ujumbe wa Vatican waishukuru Serikali ya Burkina Faso kwa kuunga mkono juhudi za Mfuko
wa Yohane II kwa ajili ya Sahel
Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki
Cor Unum na ujumbe wake kutoka Vatican, katika Maadhimisho ya Miaka 30 tangu Mwenyeheri
Yohane Paulo wa Pili alipoanzisha Mfuko wa Sahel kama sehemu ya mchakato wa kupambana
na Jangwa Barani Afrika, amemtembelea Rais Blaise Compaorè wa Burkina Faso, mjini
Ouagadogou.
Lengo la ujumbe wa Vatican kukutana na Rais wa Burkina Faso lilikuwa
ni kumshukuru kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Mama Kanisa katika mchakato wa
kuwaletea wananchi wanaoishi katika Ukanda wa Sahel maendeleo endelevu.
Serikali
ya Burkina Faso imetoa ardhi ambayo itaweza kutumika kwa ajili ya ujenzi wa Makao
ya Ubalozi wa Vatican nchini humo. Itakumbukwa kwamba, Makao Makuu ya Mfuko wa Yohane
Paulo II yako pia mjini Ouagadogou. Rais wa Burkina Faso anasema ataendelea kuunga
mkono juhudi zinazofanywa na Mfuko wa Yohane Paulo II kwa ajili ya wananchi wa Sahel,
kama kielelezo makini cha mapambano dhidi ya baa la njaa, umaskini na mardhi yanayochangiwa
kwa kiasi kikubwa na uwepo wa ukame wa kutisha.
Kardinali Sarah anabainisha
kwamba, kumekuwepo na mafanikio makubwa yaliyopatika tangu Mfuko wa Yohane Paulo II
kwa ajili ya Sahel ulipoanzishwa kunako mwaka 1983 kama njia ya kuonesha mshikamano
wa dhati na wananchi wa Ukanda wa Sahel dhidi ya ukame wa kutisha. Bado kuna mengi
yanayopaswa kutekelezwa, jambo linalohitaji mshikamano wa dhati na wadau mbali mbali
kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika.