Marufuku kuhama Ethiopia kwa kisingizio cha kutafuta fursa za ajira!
Serikali ya Ethiopia imepitisha sheria ya muda inayopiga rufuku kwa wananchi wake
kuhama kutoka nchini humo kwa ajili ya kutafuta kazi, ili kulinda usalama wa raia
wake pamoja na kuzingatia mafao ya nchi na maendeleo ya watu wake.
Wizara
ya Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa inasema kwamba, wananchi wengi
waliokufa maji hivi karibuni kwenye Visiwa vya Lampedusa, Kusini mwa Italia, ni raia
wa Ethiopia waliokuwa wanakwenda Ulaya kutafuta fursa za ajira na maboresho ya maisha,
lakini kwa bahati mbaya wamefikwa na mauti hata kabla ya kuwasili kwenye nchi husika!
Kutokana
na majanga haya yanayoendelea kuongezeka na hivyo kuhatarisha usalama wa maisha ya
wananchi wa Ethiopia, Serikali kwa muda imesitisha utoaji wa vibali kwa ajili ya watu
wanaotafuta fursa za ajira nje ya nchi. Rufuku hii itaendelea kuwepo hadi pale tatizo
hili litakapokuwa limepatiwa ufumbuzi wa kudumu. Ukosefu wa fursa za ajira miongoni
mwa vijana nchini Ethiopia ni asilimia 50%, hali inayowasukuma vijana wengi kuikimbia
nchi yao hata katika mazingira hatarishi wakiwa na tumaini la kupata walau fursa za
ajira Barani Ulaya.
Wahamiaji hawa ambao wamekuwa ni msaada mkubwa katika kukuza
na kuimarisha uchumi kwenye nchi za Falme za Kiarabu, Yemen, Afrika ya Kusini, Israel
na Ulaya. Kwa bahati mbaya, wahamiaji hawa wanakumbana na mauti hata kabla ya kutimiza
ndoto ya kupata fursa za ajira na maisha bora. Taarifa zinaonesha kwamba, baadhi yao
wamejikuta wanatumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu inayoendelea kushamiri
kwa kasi sehemu mbali mbali za dunia, jambo linalodhalilisha utu na heshima ya binadamu.