2013-10-29 08:21:33

Mapambano dhidi ya kuenea kwa Jangwa kwenye Ukanda wa Sahel ni kielelezo cha mshikamano na maskini!


Mfuko wa Yohane Paulo II kwa ajili ya Sahel ni kielelezo makini cha mshikamano wa dhati unaooneshwa na Mama Kanisa katika kupambana na uharibifu wa mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi. Hii ni huduma makini inayopania kuwajengea uwezo maskini katika mapambano dhidi ya baa la njaa, umaskini na magonjwa kwenye Ukanda wa Sahel.

Hayo yamebainishwa na wakurugenzi wa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa ajili ya Sahel katika mkutano wao wa Mwaka uliohitimishwa hivi karibuni huko Ouagadougou, Burkina Faso. Mkutano huu ulifunguliwa hapo tarehe 25 Oktoba 2013 na kuhudhuriwa na Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum.

Katika kipindi cha miaka 30 tangu Mfuko huu ulipoanzishwa, umeendelea kuwa ni alama ya mshikamano wa upendo kwa wananchi wanaounda Ukanda wa Sahel. Bodi ya wakurugenzi wa Mfuko huu wanasema, wataendeleza kazi ya kupambana na udhibiti wa kuenea kwa Jangwa katika Ukanda wa Sahel kama njia ya kumuenzi Mwenyeheri Yohane Paulo Pili katika kushughulikia "majanga" yanayomwandama mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.