Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia 2012- 2013 kukumbukwa kwa Ibada ya Misa
Takatifu, tarehe 4 Novemba 2013
Baba Mtakatifu Francisko baada ya kutembelea na kusali kwenye Makaburi ya wananchi
wa Roma kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili
alipotembelea kwa mara ya kwanza makaburi hayo sanjari na kusali kwa ajili ya kuombea
Mapapa waliotangulia mbele ya haki na kuzikwa chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
mjini Vatican, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Makardinali
na Maaskofu, Jumanne, tarehe 4 Novemba 2013.
Ibada ya Misa Takatifu inatarajiwa
kuanza hapo saa 5:30 asubuhi kwa saa za Ulaya. Hayo yamebainishwa na Mshereheshaji
mkuu wa Ibada za Kipapa Monsinyo Guido Marini siku ya Jumanne, tarehe 29 Oktoba 2013.
Mapokeo yanaonesha kwamba, Baba Mtakatifu atawakumbuka na kuwaombea Makardinali na
Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha Mwaka 2012 -2013 kutoka sehemu mbali
mbali za dunia.
Mzee mmoja wa busara anabainisha kwamba, "binadamu ana zamu
mbili duniani: kuzaliwa ni zamu ya kwanza lakini ni ya bahati nasibu. Zamu ya pili
ni mauti; hii ndiyo ya lazima na uhakika". Kila mtu ajiandae kufa kifo chema.
Mtaalam
mmoja wa mambo ya Biblia aliwahi kusema, kila mtu hujiandalia watu wa kufika msibani
mwake mwenyewe. Ukiwa na watu kwenye misiba yao ukasaidia kuwazika wafu wao, umetoa
mwaliko mzuri kwao kwa siku ya msiba wako. Kifupi, ukiwapenda watu wengi na kuwatumikia
kwa kujitolea kwao utakuwa umewapa kadi ya mwaliko nzuri ya kufika kwenye mazishi
yako. Basi wape kadi ya mazishi yako kwa kushiriki katika mahangaiko ya jirani zako!