2013-10-28 08:42:48

Utandawazi na teknolojia ya habari visiwaletee "majanga" masomoni!


Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Tanzania Dr. Rehema Nchimbi ametoa wito kwa shule zinazomilikiwa na taasisi za dini kuhakikisha zinaziba mianya yote ya mafundisho yasiyofaa kwa wanafunzi yanayoletelezwa na mabadiliko ya utandawazi ili ziweze kuzalisha wanafunzi wenye ubora kielimu na kimaadili.

Dr. Nchimbi amebainisha kuwa hivi sasa kumekuwa na mianya mingi inayowezesha mafundisho mbalimbali yanayopatikana kupitia maendeleo ya utandawazi ambayo baadhi yamekuwa na viashiria vinavyochangia kuporomoka kwa tabia, maadili na mfumo mzima wa wanafunzi kujifunza na kuwaasa wanafunzi kuwa makini sana na masuala ya utandawazi katika safari zao za masomo kwani, wasipotumia utandawazi ipasavyo itachangia kuharibikiwa katika masomo yao.

Dr. Nchimbi ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya tisa ya Sekondari ya Wasichana ya Huruma inayomilikiwa na Shirika la Watawa Wakatoliki la Misericordia iliyopo Jimbo Katoliki Dodoma ambapo mahafali hayo yalikwenda sambamba na Jubilei ya miaka 50 tangu watawa hao wa misericodia kuanza kutoa huduma za elimu nchini Tanzania.

Dr. Nchimbi ameongeza kuwa, katika ulimwengu wa sasa wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari na mawasiliano kumekuwa na matumizi mabaya ya teknolojia hizo yanayofanywa na wanafunzi, matokeo yake Jamii inazalisha wataalamu na viongozi wasiokuwa na maadili na pia amezitaka shule ningine nchini Tanzania kujipanga nazo kupambana na tatizo hili.

Mkuu wa mkoa pia ameshukuru mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini katika kuhudumia jamii akiainisha upande wa kutoa huduma za elimu kwa jamii na kusema kuwa Serikali inatambua na kuthamini sana mchango huo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hizo za kidini ili kwa pamoja waendelee kuhudumia jamii na kusaidia kuleta maendeleo ya wengi nchini Tanzania.

Kwa upande wake Askofu mstaafu Mathias Joseph Isuja wa Jimbo Katoliki Dodoma akitoa historia amesema kuwa miaka ya hapo awali mfumo wa elimu nchini Tanzania ulikuwa finyu hasa kwa upande wa wasichana kwenda shule ndipo Kanisa kupitia mashirika yake mbalimbali yakaanza kuwekeza kwenye elimu ili kumkomboa mwanadamu: kiroho na kimwili

Kwa upande wao wahitimu wa kidato cha nne wakiwakilishwa na mwanafunzi Ritah George aliyesoma taarifa ya wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimisha masomo yao ya kidato cha nne mwaka hu,u wameomba uongozi wa shule kushughulikia changamoto za maktaba yenye nafasi za kutosha, vifaa vya kujifunzia kama kompyuta, viwanja vya michezo na walimu wa michezo.








All the contents on this site are copyrighted ©.