Marehemu Askofu Mwanyika: alikuwa mcheshi, mchapakazi, mbunifu, mtu wa watu na kiongozi
aliyethubu!
Askofu mstaafu Raymond Mwanyika wa Jimbo Katoliki Njombe, aliyefariki dunia hapo tarehe
24 Oktoba 2013 anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumanne tarehe 29 Oktoba 2013.
Askofu mkuu
Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania kwa njia ya Radio Vatican anapenda
kutuma salam zake za rambi rambi kwa Askofu Alfred Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe
pamoja na Familia ya Mungu Jimboni humo. Anasema, amezipokea habari za msiba wa Askofu
mstaafu Mwanyika kwa majonzi, masikitiko na matumaini. Anaungana na Familia yote ya
Mungu nchini Tanzania kwa ajili ya kumwombea Marehemu Askofu Mwanyika ili aweze kupata
furaha ya uzima wa milele.
Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema
kuuga mfano wa huduma na majitoleo yaliyooneshwa na Marehemu Askofu Mwanyika enzi
ya uhai wake. Alikuwa ni mcheshi, mchapakazi na mbunifu. Alikuwa ni kiongozi mpenda
maendeleo, aliyebuni na kupanga mikakati ya maendeleo inayogusa mahitaji ya mtu mzima:
kiroho na kimwili. Marehemu Askofu Mwanyika, alitoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma
za kichungaji Jimboni mwake. Kwa hakika ni kiongozi aliyethubutu kutenda na kamwe
hakukata tamaa kutokana na magumu au vizingiti alivyokumbana navyo.
Askofu
mkuu Lebulu anasema, Marehemu Askofu Mwanyika alikuwa ni mtu wa watu kwa ajili ya
watu; alishiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania. Alitegemewa sana kwa ushauri wake makini na wenye busara. Askofu mkuu Lebulu
anamshindikiza Marehemu Askofu Mwanyika na Maaskofu wengine waliomtangulia katika
huduma ya Kiaskofu kwa sala na sadaka ya Misa Takatifu.