Kuna idadi kubwa ya wanawake magerezani, wanaonyanyaswa na kudhulumiwa kijinsia!
Taarifa ya Umoja wa Mataifa kuhusu makosa dhidi ya wanawake iliyotolewa hivi karibuni
inaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya wanawake ambao wako magerezani, wanadhulumiwa
kijinsia na kuishi katika mazingira hatarishi zaidi, ikilinganishwa na wafungwa wa
kiume. Hayo yamebainishwa na Bi Rashida Manjoo, mtaalam wa masuala ya wanawake, alipokuwa
anazungumza hivi karibuni kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
Vitendo vya
jinai, mmong'onyoko wa kimaadili, biashara haramu ya dawa za kulevya na ujambazi ni
kati ya makosa ambayo wanawake wengi wanashutumiwa kuyafanya na hivyo kujikuta wakiwa
wamefungwa pingu magerezani. Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha miaka ya
hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la idadi ya wanawake wanaojihusisha na
biashara haramu ya dawa za kulevya na kwamba, wengi wao wamekamatwa na kufikishwa
kwenye mkondo wa sheria na kwa sasa wanatumikia adhabu zao.
Taarifa za hali
ya wanawake magerezani zinaonesha kwamba, wanawake wanakabiliwa na hali tete ya maisha,
hii ikiwa ni nyanyaso na dhuluma za kijinsia wanapokuwa magerezani; wakati mwingine
wanalazimishwa kujihusisha na biashara haramu ya ngono. Kuna kundi kubwa la watoto
wanaoishi mama zao magerezani, hali ambayo inahatarisha malezi na makuzi ya watoto
hawa.
Mtetezi wa haki msingi za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa anasema kwamba,
kuna haja kwa Serikali kufanya upembuzi wa kina zaidi ili kubaini sababu zinazopelekea
wanawake wengi kutupwa magerezani. Serikali zinawajibu wa kulinda na kuwatetea raia
wake dhidi ya nyanyaso na dhuluma za kijinsia.