2013-10-27 11:30:48

Familia zina wajibu wa kufanya kazi, kutoa malezi na makuzi bora pamoja na kusali!


Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, katika mahojiano na Radio Vatican anasema kwamba, mwanadamu amepewa dhamana ya kushiriki katika mchakato wa kuendeleza maboresho katika kazi ya uumbaji. RealAudioMP3

Hii ni changamoto ya kutumia vyema vipaji, karama na nguvu alizo nazo kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika kazi ya uumbaji kwa vizazi vya sasa na vile vijavyo. Anakazia umuhimu wa elimu na malezi bora yanayotambua uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu na kwamba, utu na heshima ya kila mwanadamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza vinginevyo wanyonge watateseka na kudhulumiwa.

Ni vyema ikiwa kama Jamii itawajengea wanafamilia uwezo wa kufanya kazi kwa: bidii, juhudi na maarifa; kwa kupata ujira halali na unaokidhi mahitaji msingi ya familia na kwamba, familia zishiriki kikamilifu katika mchakato wa maboresho ya Jamii husika, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Familia zipate nafasi ya kupumzika na kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu. Ikumbukwe kwamba, Jumapili ni Siku ya Mungu, ni Siku ya Kristo ni Siku ya Binadamu, ni Siku ya Kanisa, ni Siku ya Mambo ya Nyakati, hapa mwanadamu anapata fursa ya kutafakari maisha ya uzima wa milele, akitambua kwamba, hapa duniani ni mpita njia, wala hana makazi ya kudumu.

Jumapili ni siku maalum inayoziwezesha familia: kusikiliza Neno la Mungu na kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, tayari kujitosa kimaso maso kueneza ushuhuda wa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.