Familia zawasha moto wa imani kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kukutana
tena Septemba 2016!
Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia anasema, Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani kwa Familia yameziwezesha familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia
kufanya hija ya maisha ya kiroho, wametambua na kuona uwepo endelevu wa Kristo aliyeteswa,
akafa na kufufuka kutoka katika wafu katika hija ya maisha yao kama ilivyokuwa kwa
wafuasi wa Emmaus.
Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanaendelea kuwaunganisha
wanafamilia, ili waweze kujisikia kuwa ni mwili mmoja na roho moja. Uwanja wa Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro kwa muda wa siku mbili umegeuka kuwa ni Emmaus ya Familia duniani,
kiasi cha kusikia uwepo endelevu wa Kristo kati yao!
Familia zinapenda kumkaribisha
Kristo kati yao ili awaangazie mwanga katika safari ya maisha yao, awasaidie nyakati
za shida na magumu; awalinde dhidi ya mawimbi mazito ya bahari; akae pamoja na wadogo
ili wazidi kukua kimo na hekima; vijana wadumu katika matumaini na kamwe wasiruhusu
watu wawapokonye tumaini hilo; wazazi wawe na ukarimu pamoja na upendo wa dhati; wazee
waonje fukuto la jirani zao.
Askofu mkuu Paglia amemhakikishia Baba Mtakatifu
kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa familia, kimekuwa ni kipindi cha sala, shangwe
na tafakari ya Neno la Mungu na kwamba, wameonja uwepo wake wa kibaba na kimama kati
yao! Kwa mara ya kwanza katika maisha na utume wake, Baba Mtakatifu Francisko amekutana
na kuzungumza na Familia.
Ni matumaini ya Askofu mkuu Paglia kwamba, wataweza
kuunganika pamoja hapo Septemba 2016 kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa.
Familia zinaporudi katika maisha ya kawaida, zinaendelea kuhamasishwa kutolea ushuhuda
wa imani kwa njia ya mshikamano wa upendo kwa kutambua umuhimu wa familia duniani.
Moto wa familia uliowashwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, utaendelea
kuenea sehemu mbali mbali za dunia.