Familia ni urithi mkubwa wa binadamu na salama ya wanyonge!
Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia akimkaribisha Baba
Mtakatifu Francisko kushiriki katika mkesha wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa ajili
ya familia, Jumamosi, tarehe 26 Oktoba 2013. Alimwonesha Baba Mtakatifu jinsi ambavyo
familia za Kikristo zilivokuwa zinafurahia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ulikuwa umesheheni wajumbe wa familia kutoka katika
nchi zaidi ya 75. Walikuwa wamekusanayika ili kuombea amani, upendo na utulivu, dhidi
ya vita, njaa na magonjwa yanayoendelea kutishia usalama wa maisha na ustawi wa familia
sehemu mbali mbali za dunia. Familia za Kikristo zilikuwa zimekusanyika kusherehekea
zawadi ya imani inayosambaratisha milima ya ubinafsi na upweke hasi na hivyo kuwafanya
kuwa ni sehemu ya Familia kubwa ya waamini ambalo ni Kanisa.
Askofu mkuu Paglia
anasema, hata katika familia za Kikristo kuna shida na mahangaiko yake, lakini hawawezi
kukata tamaa, kwa kutambua umuhimu wa familia kama kito cha thamani duniani. Ndani
ya familia humo kuna bubujika upendo unaowawezesha kuvuka vikwazo vya ubinafsi na
kuwaendea jirani zao, ili kujenga na kuimaarisha mshikamano wa upendo unaoikumbatia
dunia nzima, ili familia ziweze kuwa na umoja.
Familia za Kikristo zilizokuwa
zimekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro anasema Askofu mkuu Paglia
ni kielelezo cha mshikamano na familia zote zinazoteseka nchini Syria kutokana na
vita, ili ziweze kuonja upendo na mshikamano kutoka kwa Mama Kanisa. Familia ndio
urithi mkubwa kwa binadamu wote; ni mahali pa amani kwa wanyonge.
Familia
ndicho kiini cha uwepo wa waamini wengi kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ili kwa pamoja waweze kujenga na kuimarisha
Familia ya Watu wa Mungu, yaani Kanisa.