Kanisa kwa kuridhia itifaki ya ushirikiano na Serikali halitafuti upendeleo wa pekee,
bali kushiriki katika mchakato wa maendeleo endelevu!
Vatican na Serikali ya Equatorio Guinea, tarehe 25 Oktoba 2013 zimebadilishana hati
za maridhiano ya itifaki ya ushirikiano baina ya Serikali hizi mbili, tukio ambalo
limehudhuriwa na viongozi wa serikali na Kanisa. Ujumbe wa Serikali umeongozwa na
Rais Teodoro Obiang nguema Mbasogo na Askofu mkuu Dominic Mamberti ameongoza ujumbe
kutoka vatican katika hafla hii fupi iliyofanyika mjini Vatican.
Itakumbukwa
kwamba, kunako tarehe 13 Oktoba 2012, Vatican na Serikali ya Equatorio Guinea zilitiliana
sahihi mkataba wa ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa, mkataba ambao kwa sasa umeridhiwa
na pande zote mbili.
Itifaki ya Mkataba kati ya Serikali na Kanisa unalitambua
Kanisa kisheria na kwamba, Kanisa liko huru kutekeleza wajibu na dhamana yake ndani
ya jamii, kwa kushirikiana na Serikali kwa ajili ya mafao na maendeleo endelevu ya
wananchi wa Equatorio Guinea.
Askofu mkuu Dominic Mamberti, Katibu mkuu wa
Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican kwa niaba ya Askofu
mkuu Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, amewashukuru wadau wote waliowezesha
hatimaye, itifaki ya ushirikiano kati ya Vatican na Serikali ya Equatorio Guinea kuweza
kufikiwa baina ya pande hizi mbili. Haya ni matunda ya majadiliano ya kina kati ya
Serikali na Kanisa kwa kutambua na kuthamini mchango wa Kanisa katika mchakato wa
maendeleo endelevu kwa wananchi wa Equatorio Guinea
Hii ni huduma inayopania
maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili lakini zaidi katika sekta ya elimu na afya.
Kwa maridhiano haya, Kanisa litaweza kutekeleza dhamana na utume wake kwa ajili ya
mafao ya wengi. Kanisa halitafuti upendeleo wala faida yake binafsi, bali linapenda
kuchangia katika mchakato wa maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima:
kiroho na kimwili, likisukumwa na kipaji cha ugunduzi na huru kutekeleza wajibu huu
msingi unaopania pamoja na mambo mengine, ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika misingi
ya haki na amani.
Askofu mkuu Mamberti anasema, Kanisa litaweza kutekeleza
kwa kina zaidi dhamana hii ikiwa kama misingi iliyobainishwa na itifaki hii itazingatiwa
na kufanyiwa kazi na pande zote mbili.