Wakristo wataendelea kutangaza Injili licha ya mauaji, nyanyaso na dhuluma za kidini!
Mauaji ya viongozi wa Kanisa, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo Afrika Mashariki
ni vitendo ambavyo kamwe havitaweza kuzimisha moto na ari ya utangazaji wa Habari
Njema Afrika Mashariki na badala yake, damu ya Wakristo hao ni mbegu ya kueneza imani
sehemu mbali mbali za dunia.
Ni ushuhuda uliotolewa hivi karibuni na viongozi
wa Madhehebu ya Kikristo mjini Mombasa kufuatia tukio la mauaji ya kinyama kwa wachungaji
wawili mjini Mombasa, hivi karibuni. Viongozi wa kidini wanaitaka Serikali ya Kenya
kuhakikisha kwamba, inalinda na kudumisha uhuru wa kuabudu sanjari na utawala wa sheria.
Viongozi
hao wanasema, mauaji, mateso na dhuluma dhidi ya Wakristo hayatawafanya kuogopa kutangaza
Habari Njema ya Wokovu na badala yake, wataendelea kuchochea moto wa Injili ili watu
waweze kujenga utamaduni wa kuheshiana, upendo, haki, amani, msamaha, upatanisho na
mshikamano wa kitaifa hata katika tofauti za kidini.