Utume wa Familia kwa familia za kijeshi nchini Marekani!
Askofu mkuu Timothy Broglio wa Jimbo kuu la Kijeshi Marekani katika mahojiano maalum
na Radio Vatican anabainisha kwamba, utume wa familia ni kati ya mambo makuu yanayopewa
kipaumbele cha pekee na Jimbo lake la kijeshi linalowahudumia wanajeshi pamija na
familia zao.
Familia ni kati ya taasisi ambazo zimeathirika sana kutokana
na migogoro ya kivita na kijamii inayowahusisha wanajeshi kutoka Marekani, kwani
kutokana na kazi yao, hulazimika kuziacha familia kwa kipindi kirefu hali ambayo ni
hatari kwa ustawi na maendeleo ya familia husika. Kwa vile vita haina macho, baadhi
yao hupoteza maisha, hupata vilema vya kudumu na wakati mwingine kuchanganyikiwa.
Athari zote hizi kwa kiasi kikubwa zinabebwa na familia husika.
Anasema, kutokana
na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele kusaidia
kwa hali na mali familia zinazojikuta ziliogelea katika umaskini wa hali na kipato.
Sera ya kujali maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ni kati ya mikakati
ya Kanisa Katoliki nchini Marekani.
Huu ni mwelekeo pia unaooneshwa na Serikali
ya Marekani kwa Rais Barack Obama kumteuwa Bwana Kenneth Hackett kuwa Balozi Mpya
wa Marekani mjini Vatican. Huyu ni kiongozi ambaye kwa miaka mingi amejihusisha na
masuala ya huduma kwa maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kuteuliwa
kwake kuwa Balozi ni changamoto kwa Marekani kuonesha kwamba, inajali na kuguswa na
mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia.
Askofu mkuu Timoth Broglio
anasema, Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2016 yatafanyika Jimbo kuu
la Philadelphia, Marekani. Ni matumaini yake kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani
litajitahidi kuhakikisha kwamba, maadhimisho haya yanafanikiwa kama ilivyopangwa.
Mara ya mwisho Maadhimisho haya yalipofanyika Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia
zaidi ya waamini millioni moja walihudhuria wakati wa kufunga rasmi Maadhimisho hayo
kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa XVI.