2013-10-25 16:38:03

TRA ni "janga" la ufanisi Bandari ya Dar es Salaam


Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ameishutumu Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwa ni kikwazo kwake katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuboresha bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).

Dk. Mwakyembe alisema watu wengi wanaoitumia bandari ya Dar es Salaam (TPA) wanalalamikia madudu wanayofanya TRA hasa tatizo la kufeli kwa mfumo wa mawasiliano ya kompyuta unaotumiwa na mamlaka hiyo kutoza kodi mbalimbali.

Alitoa shutuma hizo baada ya kutakiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ajibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Watanzania wanaofanya biashara na wale wanaoishi katika jiji la Guangzhou, jimbo la Guangdong ambalo ni jiji kubwa la biashara lililoko kusini mwa China. Alhamisi, Oktoba 24, 2013 Waziri Mkuu alihitimisha ziara yake ya China kwa kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi katika jimbo hilo maarufu kwa biashara.

Bw. Stanley Mwakipesile ambaye ni mfanyabiashara wa Kariakoo anayefuata bidhaa zake katika jimbo la Guangzhou, katika hoja zake alisema utoaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam ni tatizo kubwa kutokana na mfumo wa kutoza kodi unaotumiwa na TRA kutofanya kazi siku zingine na hivyo kusababisha mteja kutozwa fedha nyingi.

Mfanyabiasahra huyo alisema kutokana na kero hiyo, wafanyabiashara wengi kutoka nchi jirani wameikimbia bandari hiyo na sasa wanatumia bandari ya Mombasa jambo ambalo alisema ni hasara kwa nchi. “Inakuwaje kila siku pale TRA system inakuwa down? Kuna urasimu mwingi tu pale lakini cha ajabu wakati wao ndio hawafanyi kazi, lakini mteja anatozwa eti kachelewesha kutoa mzigo,” alisema Mwakipesile.

Dk. Mwakyembe katika kujibu hoja za mfanyabiashara huyo alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na akasema eneo linalolalamikiwa sana ni TRA ni kuwatoza wateja tozo za ziada hata kipindi ambacho watendaji wa mamlaka hiyo hawafanyi kazi kwa kisingizio cha mfumo kutofanya kazi (system down).

“Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli TRA ni tatizo, hasa hili la system down kwa kweli ni kero na linawaumiza watu wengi wanaotumia bandari yetu. Ni lazima tukae tuone namna ya kutatua tatizo hili,” alisema Mwakyembe.

Alisema licha ya kuwepo agizo kutoka serikalini la kutaka TPA na TRA wafanye kazi saa 24, lakini watendaji wa TRA wanafanya kazi kwa saa 12 tu na wanalala kwa siku 10 katika mwezi mzima.

Alisema wakati TRA wanaenda kulala, mteja hahudumiwi na wanapokuja kuendelea na kazi kesho yake, wanawatoza wateja tozo ya kuchelewesha mzigo wakati makosa siyo ya wateja bali ni ya watendaji wa mamlaka hiyo ya kukusanya kodi kwa Tanzania. “Sisi TPA hatulali; lakini wenzetu hawa wanalala, inakuwaje wanaenda kulala wakati mizigo imerundikana pale bandarini? Kwa kweli hawa watu ni lazima tushughulike nao.

“Mimi nimesaini BRN, Rais anataka kuona mwaka 2015 shehena inaongezeka pale, na kufikia tani 18 sasa yule atakayekaa mbele yangu kunikwamisha mie nitampitia,” alisema Dk Mwakyembe na kushangiliwa kwa nguvu na watanzania hao. Hata hivyo aliwatoa hofu Watanzania kwa bandari ya Dar es Salaam inafanya kazi vizuri na kila mwaka shehena imekuwa inaongezeka, hali inayoonyesha kuwa batu nchi nyingi ikiwemo Zimbabwe bado zinatumia bandari hiyo.








All the contents on this site are copyrighted ©.