2013-10-25 16:12:00

Rais Teodor O. N. Mbasogo akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 25 Oktoba 2013 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Teodor Obiang Nguema Mbasogo kutoka Jamhuri ya Watu wa Equatorio Guinea, ambaye pia alipata nafasi ya kuzungumza na Askofu mkuu Dominic Mambert, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Viongozi hao wawili wamezungumzia mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Equotorial Guinea katika masuala ya maendeleo endelevu hususan katika sekta ya elimu, afya na utamaduni nchini humo. Kanisa limekuwa ni mdau mkubwa katika maboresho ya maendeleo ya wananchi kwa kushirikiana na Serikali.

Rais Teodor Mbasogo wamebadilishana hati za mkataba wa ushirikiano na Vatican, ili kuridhia mkataba huu uliotiwa sahihi kunako tarehe 13 Oktoba 2012 mjini Mongomo. Serikali inalitambua Kanisa kisheria; inatambua uhalali wa ndoa za Kikristo, Nyumba za Ibada, Taasisi za elimu na umuhimu wa waamini kupata msaada wa maisha ya kiroho. Mkataba huu baada ya kuridhiwa na pande zote mbili kuanzia sasa unafanya kazi rasmi.







All the contents on this site are copyrighted ©.