2013-10-25 16:06:43

Ndoa takatifu na familia inayofumbatwa katika mwanga wa Injili ni mfano wa kuigwa na wengi!


Familia ni Jumuiya ya watu inayojitegemea. Hapa ni mahali muafaka pa kujifunza kupenda na kiini cha maisha ya mwanadamu. Ni Jumuiya inayojengwa na watu wanaopendana, wanaojadiliana na kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine, ni watu wanaosimama kidete kulinda na kutetea maisha, hasa kwa wanyonge.

Familia ni kiini cha maisha na historia ya dunia. Kila mwanadamu anajenga na kuimarisha utu wake kwa njia ya familia, kwa kukua na kukomaa kama Jumuiya inayoundwa na: baba, mama na watoto. Familia ni mahali ambapo mtu anapata jina lake, mahali pa kuonjeshana upendo na ukarimu; ni mahali ambapo mchakato wa kwanza kabisa kuhusu sanaa ya majadiliano na mawasiliano ya mtu binafsi huanza kushika kasi yake.

Ni sehemu ya hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko siku ya Ijumaa, tarehe 25 Oktoba 2013 alipokutana na kuzungumza na Wajumbe wa Baraza la Kipapa la Familia ambao wako Roma kuhudhuria mkutano wa Baraza la Kipapa la Familia sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Siku ya Familia, hapo, Jumapili ijayo.

Baba Mtakatifu anasema kuwa, ni ndani ya Familia kwamba, mtu anatambua utu wake, lakini kwa namna ya pekee kwa wagonjwa, wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kutokana na ukweli huu, Familia inapaswa kutambulikana na kuheshimiwa dhidi ya haki ya mtu binafsi. Tafakari ya haki msingi za Familia iliyochapishwa hapo tarehe 22 Oktoba 1983 ndiyo iliyoongoza tafakari ya mkutano wa Baraza la Kipapa la Familia.

Baba Mtakatifu anasema, familia inasimikwa katika ndoa. Kwa njia ya pendo huru na aminifu, wanandoa Wakristo wanashuhudia ndoa kama Sakramenti ya Kanisa, msingi thabiti wa familia unaowawezesha wanandoa kujitosa kati yao bila ya kujibakiza. Ndoa inaweza kuonekana kama Sakramenti ya kwanza ya binadamu, inayomwezesha kujitambua sanjari na kufahamu uhusiano na watu wengine, upendo ambao una uwezo wa kutoa na kupokea.

Hapa waamini wanatambua wito wao wa kupenda bila kuteteleka wakati wa shida, raha na magumu, ili kuweza kukua na kudumu katika wema, ukweli na uzuri. Ndoa inamwezesha mwamini kujitosa bila ya kujibakiza kwa kushirikishana yote: zawadi na sadaka, huku wakijiaminisha kwa maongozi ya Mwenyezi Mungu. Huu ndio mwelekeo ambao vijana wanapaswa kujifunza kutoka kwa wazazi na jamaa zao.Haya ni mang'amuzi ya imani kwa Mwenyezi Mungu na hali ya kuaminiana katika uhuru wa kweli, utakatifu wa maisha, uaminifu na sadaka ya kila siku.

Baba Mtakatifu anasema, mwanadamu anapitia hatua mbili za ukuaji wake: utoto na uzee, wote hawa wanaonesha maisha ambayo ni tete na wakati mwingine yanasahaulika; kwa kufanya hivi, Jamii inaelekea katika giza na ukosefu wa dira sahihi. Huu ni ukosefu wa haki jamii na kielelezo cha kuporomoka kwa Jamii husika. Huduma kwa watoto na wazee ni kitendo cha kiungwana.

Maria na Yosefu walipokwenda Hekaluni kutolea sadaka kadiri ya sheria, walipokelewa na Mzee Simeoni na Anna, waliompokea Yesu kama Mkombozi ambaye vizazi na vizazi walisubiria huruma yake. Kanisa linalowahudumia watoto na wazee ni Mama wa vizazi yote vya waamini na mhudumu wa familia ya binadamu, ili kujenga na kudumisha upendo na mshikamano kwa wote, kielelezo cha ubaba na umama wa Mungu.

Habari Njema ya Familia ni sehemu muhimu sana ya Uinjilishaji anasema Baba Mtakatifu Francisko, ili wakristo waweze kuwasiliana na wote na kutolea ushuhuda wa maisha yao katika ulimwengu mamboleo. Familia za Kikristo zitambulike kwa uaminifu, uvumilivu, uwazi kwa zawadi ya uhai na heshima kwa wazee.

Siri ya ufahamu huu ni uwepo endelevu wa Yesu ndani ya Familia. Ndoa takatifu na familia inayofumbatwa katika mwanga wa Injili, uwe ni mfano wa kuigwa na wengi. Familia zenye matatizo zisaidiwe kuunganika, kupata kazi na faraja. Kanisa linapenda kuwa karibu na familia zote katika raha na shida zao.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mkutano wa mwaka wa Baraza la Kipapa la Familia utachangia kwa kiasi kikubwa katika Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Ndoa itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba, 2014. Mwishoni Baba Mtakatifu amewawekwa wajumbe hao chini ya ulinzi na usimamizi wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.







All the contents on this site are copyrighted ©.