Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameawaonya baadhi ya Watanzania wanaokuja katika
jiji la Guangzhou nchini China kwa ajili ya kununua bidhaa mbalimbali waache kuuza
hati zao za kusafiria kwa raia wa nchi nyingine kama njia ya kujiongeza kipato.
Ametoa
onyo hilo Alhamisi, Oktoba 24, 2013 wakati akizungumza Watanzania wanaofanya biashara
na wale wanaoishi katika jiji la Guangzhou, jimbo la Guangdong ambalo ni jiji kubwa
la biashara lililoko kusini mwa China.
Alisema kuwa wengi wa wafanyabiashara
hao wanapouza pasipoti zao wanasingizia kuwa zimepotea ndio maana kuna malalamiko
mengi kutoka kwa Watanzania wanaofika katika jimbo hilo kudai wanaibiwa hati zao za
kusafiria wakati sio kweli. Wakati wa mazungumzo hayo, mmoja wa Watanzania hao aliyejitambulisha
kwa jina la Ambrose Lugai alisema changamoto nyingi zinazowakabili Watanzania waishio
katika jimbo hilo na moja ya tatizo hilo ni kuibiwa kwa hati za kusafiria za Watanzania.
Bw.
Lugai alisema tatizo la wafanyabiashara wengi kupoteza pasipoti limekuwa sugu na kila
siku linaongezeka na cha ajabu linawatokea wafanyabiashara wa kutoka Tanzania tu.
“Hatuwezi kusema ni u-carelessnes, lakini jamii ya hapa ni kutoka mataifa mbalimbali,
inakuwaje pasipoti za Tanzania tu ndio zinakuwa hot cake, naomba utusaidie namna ya
kulinda hati hizi,” alisema Bw. Lugai.
Alimwomba Waziri Mkuu awasaidie kuzungumza
na Serikali ya jimbo hilo ili Watanzania wawe wanaacha pasipoti hotelini wakati wanapoenda
mitaani, badala yake wapewe karatasi nyingine ya kuwatambulisha huko mitaani.
Katika
kujibu hoja hiyo ya Bw. Lugai, Waziri Mkuu alisema kwamba suala hilo linamshangaza
kwamba inakuwaje hati za wafanyabiashara wa Tanzania tu ndio zinaiibiwa wakati wafanyabiashara
wanaofika kwenye jimbo hilo ni wengi kutoka mataifa mbalimbali. “Kupoteza pasipoti
ni jambo la nadra sana, sio la kawaida. Nilitegemea hili linaweza kumtokea mtu mmoja
mmoja, lakini nashangazwa kwamba hapa Goangzhou ni tatizo kubwa.”
“Lakini taarifa
nilizo nazo nyie wenyewe wafanyabiashara mnauza hati zenu kwa Wanaigeria ili mpate
fedha za kufanyia biashara. Ndio maana nawasihi achani haya mambo, mnajifedhehesha
wenyewe na mnaifedhehesha nchi,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema kwa kuwa tatizo
hilo ni kubwa na akamtaka balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali mstaafu
Abdulrahman Shimbo afuatilie kwa karibu kujua idadi ya watu walioibiwa hati zao za
kusafiria ili Serikali iweze kulishughulikia. “Lakini nawaonya acheni tabia mbaya
ya kuuza pasipoti zenu kwa tamaa ya kupata vijipesa vidogo vidogo hivyo, hii ni kuivunjia
nchi heshima,” alisema.
Lakini pia alitaka jumuiya ya Watanzania waishio China
kuimarishwa zaidi ili wawe na uwezo wa kushughulikia kero zao mbalimbali zinazowakabili
wakiwa katika ugenini. Alisema ni kuimarika kwa jumuiya hiyo tu kutawasaidia wanafunzi
na wafanyabiashara kufikisha malalamiko yao haraka serikalini.