Familia inapaswa kulindwa, kutetewa na kuhifadhiwa kwa haki na nguvu zote!
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa ajili ya Familia, Askofu Telesphor Mkude
wa Jimbo Katoliki Morogoro, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Familia, Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania anakiri kwamba, familia ni tunu ya pekee katika maisha
ya mwanadamu ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, hali inayoonesha ule utukufu
wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Utukufu huu
umechafuliwa kutokana na uwepo wa dhambi ya asili pamoja na mapungufu yanayoendelea
kujitokeza katika maisha ya mwanadamu.
Mwanaume na mwanamke wameumbwa na Mungu
ili waweze kukamilishana, kusaidiana na kutakatifuzana katika hija ya maisha yao hapa
duniani. Kilele cha kazi ya uumbaji ni mwanadamu anayeshiriki dhamana na wajibu wa
kuendeleza kazi ya uumbaji iliyoanzishwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Kutokana na wajibu
huu, zawadi ya uhai inapaswa kulindwa na kutetewa tangu pale mimba inapotungwa.
Ikumbukwe
kwamba, mtoto ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hata familia zile ambazo
hazijabahatika kupata watoto, wao kimsingi wanaunda familia. Askofu Mkude anasema,
hakuna mtoto anayezaliwa kwa bahati mbaya. Sera na mikakati inayolenga kudhibiti na
kukumbatia utamaduni wa kifo inakwenda kinyume kabisa cha mpango wa Mungu katika maisha
ya mwanadamu. Hiki ni kielelezo cha ubinafsi wa hali ya juu kuliko maendeleo, tija
na ustawi wa mwanadamu.
Familia inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika
mikakati, mipango na sera za Serikali na wadau mbali mbali. Familia ipewe heshima
na haki zake msingi; itambuliwe na kuthaminiwa. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto katika
mahubiri yake kwenye Siku ya Familia Kimataifa iliyofanyika Jimbo kuu la Milano, Kaskazini
mwa Italia na kuhudhuriwa na bahari ya wanafamilia kutoka sehemu mbali mbali za dunia
alisema kwamba, familia inapaswa kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa
dhati.
Serikali na watunga sera wajitahidi kuenzi tunu msingi za maisha ya
kifamilia; familia ipewe haki ya kuishi kwa pamoja; iwe na uhuru wa malezi na elimu
kwa watoto wake. Kwa maneno mengine familia inapaswa kulindwa, kutetewa na kuhifadhiwa
kwa haki na nguvu zote. Askofu Mkude anasema, familia inapaswa kupewa fursa ya kufanya
kazi ili iweze kutekeleza dhamana na wajibu wake.