Epukeni kuwa ni watumwa wa dhambi! Msipindishe majina ya dhambi kukwepa ukweli!
Wakristo wanapaswa kujenga ujasiri, ukweli na uwazi wa kuungama dhambi zao bila kuogopa
wala kuficha jambo lolote kama njia ya kuonja tena huruma na upendo kutoka kwa Yesu
Kristo na kwa njia hii waamini wanaweza kugundua tena huruma ya Mungu katika maisha
yao.
Kuna baadhi ya waamini wanapata shida sana kwenda kuungama dhambi zao
mbele ya Padre, hali ambayo inadhohofisha umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho miongoni
mwa waamini.Mtakatifu Paulo anapowaandikia Warumi anasema kwamba, dhambi iliyoko ndani
mwake ndiyo inayompelekea kutenda kinyume cha utashi wake. Haya ni mambo yanayojitokeza
katika maisha ya imani, kwani ubaya bado unamwandama mwanadamu.
Hayo yamesemwa
na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu
Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 25 Oktoba 2013. Anawahimiza waamini
kupambana kufa na kupona dhidi ya dhambi, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu katika
maisha yao. Waamini wajifunze kuepuka kuwa ni watumwa wa dhambi kwa kumpatia Yesu
nafasi katika mioyo na maisha yao; wawe na ujasiri wa kuiita dhambi kwa jina kamili
na wala si kwa kuipachika majina ya bandia, kwani hiki ni kielelezo cha unyenyekevu
mbele ya Mwenyezi Mungu.
Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuungama
dhambi zao, ili kumpatia Mwenyezi Mungu utukufu kwani Yeye ndiye anayemkomboa mwanadamu
kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu anasema, mwamini hawezi kuungama
dhambi zake kwa njia ya mitandao ya jamii, bali ni kumwendea Kristo kwa kutambua kwamba,
yeye ni mdhambi mbele ya Padre ambaye ni Wakili wa Kristo.
Waamini wawe na
unyenyekevu wa kuona ubaya wa dhambi ili waweze kutubu na kuungama mbele ya Mwenyezi
Mungu. Wawe wakweli, wa wazi na wanyenyekevu kama watoto wadogo. Kumwonea Mungu aibu
ni kielelezo cha neema, kama alivyofanya Mtakatifu Petro, alipokutana na Yesu, akajiona
mtupu mbele ya utakatifu na ukuu wa Kristo.