Sh. Trilioni 2.72 kuwekezwa kwenye ujenzi wa miradi ya umme, nyumba za makazi ya watu
na biashara!
Serikali ya Tanzania imeingia mikataba saba na makampuni sita ya Kichina yenye thamani
ya dola za Marekani bilioni 1.7 (Sh. trilioni 2.72) ambazo zitawekezwa kwenye ujenzi
wa miradi ya umeme na nyumba za makazi na biashara.
Makubaliano ya uwekezaji
huo mkubwa yameshuhudiwa Alhamisi, Oktoba 24, 2013 na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na
mawaziri wengine wa Serikali baada ya kusainiwa kwa mikataba saba ya uwekezaji katika
sekta hizo muhimu kwa uchumi wa nchi.
Utiaji saini huo ulifanywa mara baada
ya Waziri Mkuu kufungua Kongamano la Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na China
(Tanzania China Business Forum) uliofanyika kwenye hoteli ya Dong Fang, jijini Guangzhou
jimboni Guangdong, China. Kongamano hilo ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano kati
ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Baraza la Biashara la China Afrika (China
Africa Business Council-CABC) linashirikisha wafanyabiashara wa China na Tanzania.
Mikataba
iliyosainiwa leo ni kati ya Shirika la Umeme (Tanesco) na Kampuni ya Tabiau Electric
Apparatus Stock Co Ltd (TBEA) ambao ni kwa ajili ya ujenzi wa njia ya umeme ya msongo
mkubwa wa 400kV katika Gridi ya Taifa inayotoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kaskazini
Mashariki hadi Arusha.
Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO, Bw. Felchesmi Mramba ndiye
aliyesaini mkataba huo wenye thamani ya dola za marekani milioni 692.7. Bw. Mramba
pia alisaini mkataba mwingine na kampuni ya Shanghai Electric Power ambayo ndio itajenga
mtambo wa Kinyerezi III.
Mkataba mwingine uliotiwa saini na Mramba ni kati
ya Tanesco na kampuni ya China Gezhouba Group Corporation (CGGC) ambao wamekubali
kuendeleza mradi wa umeme unaotokana na nguvu ya maji wa Rumakali ambao uko katika
mikoa ya nyanda za juu kusini. Miradi hiyo miwili bado iko kwenye ngazi ya upembuzi
yakinifu hivyo gharama zake bado hazijajulikana.
Kampuni ya Mkonge Energy Systems
Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara wa Tanzania, Bw. Salum Shamte ilitiliana saini
mkataba na kampuni ya Sino Hyro Resources Ltd kwa ajili ya kuendeleza umeme wa nguvu
za maji wa Masigira. Mradi huo unagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 136.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Nehemia Mchechu aliweka saini
mkataba baina ya NHC na kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE) kwa
ajili ya kuliwezesha kifedha shirika hilo liweze kujenga nyumba mbalimbali za makazi
na biashara nchini. Mradi huo una thamani ya dola za Marekani milioni 500.
Bw.
Mchechu pia aliwekeana saini mkataba mwingine na kampuni ya Poly Technologies (POLY)
wa kuwa na uhusiano kifedha na kiufundi kati ya kampuni hizo ya kichina na NHC kwa
ajili ya kujenga nyumba za makazi na biashara huko Masaki wilaya ya Kinondoni jijini
Dar es Salaam. Gharama za mradi huo ni dola za Marekani milioni 200.
Mkurugenzi
wa Shirika la Maendeleo (NDC) Bw. Gideon Nassari kwa niaba ya shirika lake aliingia
mkataba na kampuni ya China ya Dalian International Economic & Technical Gooperation
Group (CDIG) na Kampuni ya Hydro China Kunming Engineering Corporation kwa ajili ya
kujenga kituo cha utafiti na mafunzo ya nishati mbadala. Mradi huo una thamani ya
dola za Marekani milioni 136.
Mramba na Mchechu kwa nyakati tofauti walisema
kwamba utekelezaji wa miradi hiyo utaanza wakati wowote kwani mambo mengi walishayakamilisha
kwenye mazungumzo.
Wakati utambulisho, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bibi Julieth
Kairuki alisema jumla ya Makampuni na Taasisi 46 zinazowekeza na kufanya biashara
Tanzania zinashiriki katika Kongamano hilo ambapo kwa upande wa China, CABC wameandikisha
makampuni 44 yatakayoshiriki kwenye kongamano. Katika Kongamano hilo, TIC imewasilisha
mada ya mazingira ya uwekezaji Tanzania na Bodi ya Utalii na Shirika la nyumba la
Taifa wamewasilisha mada zinazohusu uwekezaji kwenye sekta ya Nyumba na fursa za utalii
nchini Tanzania
Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya nane ya ziara yake
ya kikazi kwa mwaliko wa Serikali ya China bado anaendelea na mikutano mbalimbali
na leo usiku atazungumza na Watanzania waishio Guangzhou.