2013-10-24 09:06:34

Millioni 72 zatolewa na Cor Unum kwa ajili ya wananchi wa Syria


Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum limetoa kiasi cha dolla millioni 72 kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma za kibinadamu nchini Syria. Hadi sasa kuna Mashirika 32 ya Misaada ya Kanisa Katoliki yanayowahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria wanaoishi huko Lebanon, Yordani, Uturuki, Iraq, Cyprus na Misri. Hizi ni juhudi za Cor Unum zilizopitishwa katika mkutano wake uliofanyika hapo tarehe 4 hadi 5 Juni 2013.

Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akifuatilia kwa ukaribu sana matukio mbali mbali yanayoendelea kujitokeza nchini Syria. Amekazia umuhimu wa Kanisa kuchangia katika huduma kwa watu walioathirika na vita bila ubaguzi wala upendeleo, ili hatimaye, kujenga na kuimarisha Jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa.

Caritas Mashariki ya Kati imekabidhiwa dhamana ya kuratibu misaada ya Kanisa Katoliki kwa ajili ya wananchi wa Syria ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na mgogoro wa kivita unaoendelea nchini humo. Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki huko Mashariki ya kati yamehamasishwa kushirikiana kwa dhati katika kuwafikia walengwa kwa kuwa na takwimu sahihi.







All the contents on this site are copyrighted ©.