2013-10-24 08:50:07

Mapadre na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani


Kardinali Mauro Piacenza, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri hivi karibuni amezungumzia kuhusu: toba na wongofu wa Makleri katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, akichambua kwa namna ya pekee umuhimu wa Makleri kufanya toba kama msingi thabiti unaowawezesha Makleri kuwaimarisha ndugu zao katika imani. Kardinali Piacenza alikuwa anazungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. RealAudioMP3

Daraja takatifu la Upadre linawawezesha mapadre kupokea chapa ya Roho Mtakatifu inayowawezesha kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Hapa ni mahali ambapo, imani inapyaishwa tena kadiri Padre anavyojiweka mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa toba na wongofu wa ndani, jambo ambalo linamwezesha kuzaa matunda ya ajabu katika maisha na utume wa Kanisa.

Yote haya yanawezekana ikiwa kama Padre ana imani madhubuti na anatambua kile anachopaswa kutenda na anakitenda kwa ari na moyo mkuu. Mapadre watambue kwamba, wao kimsingi ni watu wa imani, waliopewa dhamana ya kuwaimarisha ndugu zao katika Kristo ndani ya Kanisa kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Jambo hili ni muhimu sana katika ulimwengu wa utandawazi ambamo ubinafsi unaonekana kushika kasi ya ajabu, Mapadre wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wakitumbukia katika ubinafsi kutokana na ubinadamu wao na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu na dhamana waliyokabidhiwa na Mama Kanisa walipopewa Daraja Takatifu la Upadre.

Kardinali Piacenza anasema, Mapadre wanayo dhamana ya kuwahudumia Watu wa Mungu kiroho na kimwili: kwa njia ya huduma mbali mbali za kijamii sanjari na Uinjilishaji, kwani kwa njia ya Fumbo la Umwilisho; Neno wa Mungu amejifanya mtu, katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Toba na wongofu kwa Mapadre wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, ni changamoto kwa Makleri kusimama kidete katika imani, huku wakiwa na ari mpya katika maisha yao ya kiroho yanayowasukuma kuwaimarisha ndugu zao katika Kristo, kama dhamana waliyokabidhiwa na Mama Kanisa.

Wahakikishe kwamba, wanatumia nyenzo mbali mbali zilizoko mbele katika kutekeleza wajibu huu msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Makleri ni vyombo vya Roho Mtakatifu katika kuwatakatifuza Watu wa Mungu, ndiyo maana kuna uhusiano wa karibu kabisa kati ya toba, wongofu wa ndani, karama za Roho Mtakatifu na utume wanaopaswa kuutekeleza kwa niaba ya Mama Kanisa.

Kardinali Mauro Piacenza anawaalika Mapadre kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, huku wakiendelea kuijenga na kuiimarisha kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu, Matendo ya toba na huruma. Huduma kwa Familia ya Mungu, ipewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Mapadre, wakitambua kwamba, hata wao, Mwenyezi Mungu anawasubiri kuona wakifanya hija ya toba na wongofu wa ndani kwa unyenyekevu na moyo mkuu.

Kama binadamu wana utajiri mkubwa lakini pia wanayo mapungufu yao yanayoweza kuwa ni kikwazo katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, kumbe, toba na wongofu wa ndani ni jambo la msingi, linalowawezesha kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, tayari kuwaimarisha ndugu zao katika imani.

Mapadre wakumbuke kwamba, utume wao ni mtakatifu, lakini umewekwa kwenye chombo cha udongo kinachohitaji uangalifu mkubwa, ili kutekeleza na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa unyenyekevu, huku wakitafakari kazi ya Mungu inayowaalika, inayowapatia nafasi ya kufanya toba na kuchuchumilia wongofu wa ndani; kwani neema ya Mungu inaponya na kutakatifuza.

Ni mwaliko wa kumtangaza Mwenyezi Mungu ambaye wamemtafakari, wakamwona na kumwadhimisha; huyu ndiye Neno wa Mungu aliyejifanya mtu! Kwa kutambua ukuu wa Yesu Kristo kama Mkombozi wa dunia; aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu; Kuhani mkuu wa Agano Jipya na la Milele; Mwaka wa Imani unakuwa ni hazina kubwa kwa Mapadre kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo.

Kardinali Mauro Piacenza anaendelea kufafanua kwamba, utekelezaji wa majukumu ya maisha na wito wa Kipadre kwa uaminifu, unyenyekevu na moyo mkuu ni jambo ambalo linaleta furaha kwa Mapadre ili kuwaimarisha ndugu zao katika Kristo. Toba na wongofu wa ndani kwa Mapadre ni chumvi na mwanga unaoimarisha na kukoleza imani ya Wakristo, vinginevyo, kashfa na mmong’onyoko wa kimaadili vinaweza kutjitokeza na kuwa ni kikwazo kikuu kwa maisha na utume wa Kipadre.

Kuna haja kwa Mapadre katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kutambua, kukiri na kuimwilisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Imani iwe ni utambulisho wa Mapadre katika maisha yao. Imani na toba ni chanda na pete katika maisha na utume wa Mapadre anasema Kardinali Piacenza.

Ili kutekeleza dhamana na wajibu wa kuwahudumia wengine katika imani, kunahitaji ushuhuda wa maisha hasa kutokana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni wajibu unaotekelezwa katika ngazi ya mtu mmoja mmoja au kama Jumuiya ya waamini.

Wito na dhamana waliyokabidhwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni jambo ambalo linawataka Mapadre kufikiri na kutenda kadiri ya wito wao. Ushuhuda wa maisha yao, uwe ni mfano bora wa kuigwa na wale wanaowazunguka na kamwe wasiwe ni sababu ya kashfa na kuanguka kwa Wakristo. Wawe ni viongozi wenye msimamo imara na dira makini ya kufuatwa. Daima waendelee kujifunza kutoka katika shule ya Mama Bikira Maria, aliyefanikiwa kusikiliza kwa makini, akafanya uamuzi wa busara na kutenda kwa hekima kadiri ya Mpango wa Mungu katika maisha yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.,
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.