2013-10-23 09:05:32

Wito ni alama ya matumaini katika msingi wa imani


Wito wa maisha ya upadre na maisha ya wakfu hutokana na makutano binafsi kati ya mtu na Kristo, katika uwazi na ukweli na hutualika kuingia katika mapenzi yake. Na yule anayeitikia anaingia katika mapendo yasiyo na masharti na Mungu anayemwita. Ni maneno ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa XVI – katika siku ya Miito Duniani kwa mwaka 2013 anayewashirikisha waamini tafakari hii: kuhusu matumaini na imani kama chanzo cha wito.

Ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Padre Reginald Mrosso, mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania wakati alipokuwa anazindua mwaka wa malezi ya kwanza na yale ya pili kwa Waseminari wa Shirika la Damu Takatifu Yesu, Jimboni Dodoma, sanjari na Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo hapo tarehe 21 Oktoba 2013.

Anasema, matumaini ni matarajio ya jambo jema lijalo na wakati huo huo linashikilia hali ya sasa, ingawa zaweza kuwepo hali za kukata tamaa na kushindwa. Matumaini yetu yameshikiliwa na nini? Historia ya taifa la Israeli yatuonesha jambo ambalo hujirudia mara nyingi, na hasa wakati wa magumu kama wakati wa Kutoka utumwani, na tunaona katika maandiko hasa ya Manabii:kumbukumbu ya ahadi kwa mababu; kumbukumbu hii hutualika kuwaiga mababu kama Abrahamu ambaye kama aandikavyo Mtume Paulo katika Barua kwa Warumi – imani, utajiri wa maisha anasema: Abrahamu aliamini kupita matumaini kwamba angekuwa Baba wa taifa – Rom. 4:18, kinyume cha matumaini, alitumaini na kusadiki, kwamba atakuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyosemwa, hivyo ndivyo wazao wako watakuwa wengi.

Jambo la uhakika na tulizo kubwa linaloonekana katika historia ya ukombozi ni uaminifu wa Mungu kwa ahadi alizofanya na watu wake, akilihuisha mara nyingi hata pale mwanadamu alipotenda dhambi dhidi ya agano – angalia tangu wakati wa gharika – Mwa. 8:21-22, kutoka na safari ya jangwani – Kum. 9,7 – kumbuka wala usisahau kwamba ulimkasirisha Bwana Mungu wako huko jangwani. Toka siku ile ulipotoka nchi ya Misri mpaka ulipofika mahali hapa, umekuwa ukimwasi Bwana.

Ni uaminifu huu wa Mungu uliopelekea kufanya agano jipya na mwanadamu, kwa njia ya mwanae, aliyekufa na kufufuka kwa ajili ya wokovu wetu. Hata katika nyakati za dhiki kuu, uaminifu wa Mungu umebaki na kuongoza historia yetu ya wokovu, ambayo hugusa mioyo ya watu na kuwaimarisha katika hilo tumaini la kuweza kufika siku moja nchi ya ahadi. Huu ndio msingi halisi wa matumaini, iwe hasi au chanya – Rejea Zaburi. 62;6 – ee nafsi yangu, upumzike katika Mungu tu, maana tumaini langu latoka kwake.

Kuwa na matumaini maana yake ni kumwamini Mungu ambaye ni mwaminifu, anayeshika ahadi za agano. Imani na matumaini kwa hiyo vinahusiana kwa karibu. Matumaini ni neno kuu katika imani ya kibiblia, kiasi kwamba matumaini na imani huelezwa kama kitu kimoja. Katika barua kwa Ebr. 10;23 – na tuyashike matumaini tunayoungama bila kusitasita, kwa maana yeye aliyetoa ahadi ni mwaminifu na imani kamili Ebr. 10:22- kwa hiyo tujongee kwa mioyo minyofu na imani kamili, maana mioyo yetu imenyunyiziwa na kusafishwa na dhamiri mbaya na miili yetu imeogeshwa katika maji safi.

Kwa njia ya Roho Mtakatifu – Rom. 5,5 – matumaini yetu yanadumu kwa sababu chanzo chake ni Roho Mtakatifu na tumepokea upendo – 1Yoh. 4;16 – tumeona na kugusa uwepo wake Mungu. Huu ndio upendo wa kweli, unaopenya ndani kabisa ya maisha yetu. Ni pendo linalodai mno na mwanadamu anayeongozwa na upendo wa Mungu huitwa kujibu. Ndiyo maisha ya wito.

Padre Mrosso anasema, Maisha ya wito – maana yake ni maisha ya kumfuata Mungu na ni itikio la mtu katika uhuru wake akimfuata Roho wa Mungu na akitaka kutimiza mapenzi ya Mungu Baba. Historia ya kanisa inaongozwa na Mungu mwenyewe anayemwita mwanadamu na kumtuma aende akafanye kazi aliyomwagiza. Yafaa nini mtu kuupata ulimwengu wote na kuiangamiza nafsi yake? Matayo 19,16.

Katika imani, zawadi ya Mungu, tunatambua upendo mkubwa kabisa wa Mungu kwa njia ya mwanae, Yesu Kristo na Roho Mtakatifu ambaye hututakatifuza, huangazia maisha yetu yajayo na hutujalia nafasi ya kuwa wapya tukiwa na matumaini na tukiwa na furaha. No. 7 – MWANGA WA IMANI.

Imani hufungua njia ya matembezi na kutuongoza katika histori ya maisha yetu. Na ili kuweza kuelewa imani ni nini, hatuna budi kukumbuka ule mzunguko wake, njia ya wanadamu waamini, kama tunavyoona katika Agano la Kale. Kwa namna ya pekee tunamwona Abrahamu, Baba yetu wa imani. Anapewa jukumu maalumu. Mungu anamwita, anajifunua kama Mungu anayeongea naye na anayemwita kwa jina.

Imani huendana na kusikiliza/kusikia. Jambo hili ni muhimu sana – ni lazima kusikia kwa akili, kwa moyo na kuamini. Abrahamu hakumwona Mungu, lakini anasikia sauti yake. Kwa njia hii, imani huchukua nafasi/tabia/hali ya nafsi ya mwanadamu. Hivyo Mungu huyo hafungwi na wakati, nafasi, mahali n.k bali huhusianishwa na mtu, (kama ninyi leo – Mungu anawaita kwa majina yenu na kwa kuitikia – Mungu anatukuzwa) Mungu wa Abrahamu, Isaka, Yakobo na anafanya agano na mtu. Imani huwa ni jibu kwa Neno hilo la Mungu kwake yeye anayeongea nasi. Na. 8 – Mwanga wa Imani.

Ninyi pia leo mnaingia kwa namna ya pekee katika mzunguko huo wa mpango wa Mungu wa ukombozi. Vueni utu wa kale – vaeni utu mpya – Efe. 4:22.... Mtakatifu Gaspar alivaa kanzu la kifrateri akiwa na miaka 10. Rejea. St. Gaspar, saint of the People – pg. 16.

Mtume Petro – anatualika tuingie katika maatumaini mapya – 1Pet. 1: 13-21 – matumani yanayopaswa kubadili maisha – kwa hiyo fungeni mkanda viuno vyenu muwe tayari rohoni mwenu. Muwe na kiasi. Kwa moyo wote itegemeeni neema mtakayoletewa siku ya kufunuliwa Yesu Kristo. Muwe watoto watiifu. Msifuate tena tamaa zenu kama wakati mlipokuwa hamjui bado kitu. Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, hivyo yawapasa ninyi pia kuwa watakatifu katika mwenendo wenu wote.

Kwa maana imeandikwa: muwe watakatifu kwa kuwa mimi nilivyo mtakatifu. Ikiwa mnamwita Baba yeye amhukumuye kila mtu bila ubaguzi kadiri ya matendo yake, imewapasa kuenenda kwa uchaji wa Mungu muda wa kukaa kwenu hapa ugenini. Mmejua kwamba hamkufidiwa kwa vitu vinavyoharibika kama fedha au dhahabu katika mwenendo wa upuzi mlioupokea kwa baba zenu, bali mmefidiwa kwa damu azizi ya mwanakonodoo asiye na ila wala waa, ndiyo ya Kristo. Huyo ameteuliwa tangu kabla ya kuumbwa ulimwengu, lakini amefunuliwa mwisho wa nyakati kwa ajili yenu. Kwa ujumbe wake yeye mnasadiki kwa Mungu aliyemfufua katika wafu na kumpa utukufu, mpate kusadiki na kumtumainia Mungu.

Mtakatifu Gaspari del Bufalo alitambua vizuri kabisa mpango huu wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu na akaingia katika falsafa hii ya Mungu. Aliweka katika matendo ufahamu huo akitoa ushuhuda na hata kumwaga damu yake kama Kristo kwa ajili ya ndugu zake. Leo tunakaa hapa pamoja kusali na kutafakari juu ya ukuu huu Mungu na upendo wake kwetu lakini zaidi pia tunatafakarishwa juu ya wajibu wetu mbele ya Mungu na watu wake.

Jikabidhimini daima kwa Mungu – kwa maana ni Mungu anayewawezesha ninyi kutaka na kutenda yanayompendeza yeye – Fil.2:13. Msitegemee msijitegemee wenyewe bali jikabidhini kwake Mungu. Wekeni matumaini yenu yote kwa Mungu. Katika 1Pt. 3:15 – tunasoma hivi – mtukuzeni Kristo Bwana mioyoni mwenu. Daima muwe tayari kumjibu kila mtu nayewauliza habari za matumaini mliyo nayo.

Na ili kuweza kutoa majibu ya matumaini yenu hamna budi kuishi maisha ya ushuhuda wa kweli. Deni mlilo nalo toka sasa na kuendelea ni maisha ya ushuhuda kamili.








All the contents on this site are copyrighted ©.