2013-10-23 15:15:41

Vyuo vya ufundi ni viwanda vya ajira kwa vijana!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na serikali yake wameombwa na Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi (VETA) nchini kuangalia upya na kwa haraka, umuhimu wa kuifanya marekebisho Sheria ya Manunuzi nchini kwa sababu sheria hiyo katika hali yake ya sasa inarudisha nyuma maendeleo ya VETA na taasisi nyingine nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Eng. Zebadayo Moshi amemwambia Rais Kikwete, Jumamosi, Oktoba 19, 2013, kuwa ni vigumu kwa VETA kulazimika kwenda makampuni ya Toyota ama Scania kila mara kununua magari mapya kwa ajili ya mafunzo ya wanafunzi wao kwa sababu Sheria hiyo inazuia taasisi za umma kununua na kutumia vifaa vilivyokwishatumika.

Mkurugenzi huyo alikuwa akizungumza leo kwenye Sherehe ya Ufunguzi wa Kituo cha Mafunzo ya Ufundi cha Wilaya ya Makete (MDVTC) cha VETA, mjini Iwawa, mji mkuu wa Wilaya ya Makete, ambako Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi na ambaye amefungua rasmi Kituo hicho.

Amesema Eng. Mosha: “Sheria hii ya manunuzi itaua kabisa shughuli za VETA na taasisi nyingine za umma nchini. Sisi siku zote, tunafundisha kwa vitendo na hivyo tunapotaka kumfundisha mwanafunzi gari ni lazima tuwe na gari ama jinsi injini ya gari inavyofanya kazi ni lazima tuwe na injini. Lakini kwa sababu Sheria hii inatuzuia kununua vifaa vilivyotumika, tunalazimika kwenda Toyota ama Scania kununua gari jipya ama injini ya gari mpya. Hili litatufikisha mbali kweli?”

“Majuzi tumeanzisha mafunzo ya ndege na injini za ndege zinavyofanyakazi na kwa sababu ya Sheria hii ni lazima twende Kampuni ya Boeing ya Marekani kununua injini ya ndege hiyo,” amesema kuwa wananchi walioshiriki sherehe hiyo wakiangua vicheko.

Rais Kikwete amemwambia Mkurugenzi Mkuu huyo wa VETA: “Nimesikia. Tutazungumza na wahusika kuona nini kinaweza kufanyika. Tulipata kujaribu kuifanyia marekebisho sheria hii lakini wakubwa wale wakakataa na kuruhusu taasisi moja tu ya Serikali kuweza kununua vifaa vilivyokwishakutumika.”

Kituo hicho cha Ufundi cha VETA cha Wilaya ya Makete ni cha kwanza cha aina yake kujengwa nchini kwa sababu ni cha kwanza kujengwa kwa dhana ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM mwaka 2013 ambayo iliahidi kuanza kujenga vyuo vya ufundi katika wilaya badala ya mikoa.

Aidha, Kituo hicho ni cha kwanza cha aina yake nchini kwa kuwa kimejengwa na wanafunzi na wakufunzi wa Chuo cha VETA Mpanda, Mkoa wa Katavi, jambo ambalo limeokoa gharama za ujenzi kwa kiasi cha Sh. bilioni 1.45 pamoja na kwamba mchanga wa ujenzi uliokuwa unachukuliwa kutoka Makambako, mji mwingine wa Mkoa wa Njombe kwa sababu Makete hakuna mchanga unaofaa kwa ujenzi wa mithili ya chuo hicho.

Chuo hicho ambacho ujenzi wake ulianza Aprili 27 mwaka huu kwenye eneo la Kituo hicho la ekari 124 tayari kina wanafunzi 37 wanaoshiriki mafunzo ya ufundi ya ushonaji na uashi wakiwa ni miongoni mwa wanafunzi 145,511 ambao wanaendelea na mafunzo katika vyuo vya ufundi pote nchini.

Akizungumza na wananchi baada ya kufungua Kituo hicho cha kisasa na cha kuvutia, Rais Kikwete ameipongeza VETA kwa kujenga chuo hicho cha kwanza kwa dhana mpya ya kufikisha elimu ya ufundi wilayani.

Rais Kikwete pia ameitaka VETA kuendelea kutoa mafunzo kulingana na mahitaji ya eneo husika na kutumia raslimali zinazopatikana katika eneo ambako chuo kipo na kwa Mkoa wa Njombe amesema kuwa anataraji kuwa VETA itajiekeleza katika ufundi unaohusiana na mazao ya mbao na wa viazi mviringo. “Uhodari wa watu wa Makete hauwezi kuendelea kuwa kupanga viazi ama mbao tayari kuzipeleka sokoni Dar Es Salaam, Uhodari sasa uwe ni wa kuanzisha viwanda vya fenicha baada ya vijana wenu kupata mafunzo katika Kituo hiki ama kutengeneza mapochopocho yanayotokana na viazi. Tunahitaji siku moja na sisi kusema kuwa fenicha hii safi imetengenezwa Makete.”

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa VEAT iangalie uwezekano wa kuwapatia wahitimu wake zana na vifaa vya kuanzia kazi za kujitegemea baada ya kumaliza mafunzo yao. “Lazima vijana hawa tuwasaidie kujiajiri kwa sababu tunahitaji sana mafundi stadi na mafundi mchundo kuongeza thamani kwenye uchumi wetu.”

Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku saba kukagua na kuzindua shughuli za maendeleo katika Mkoa wa Njombe








All the contents on this site are copyrighted ©.