2013-10-23 08:32:59

Umuhimu wa Neno la Mungu katika Familia


Maandiko Matakatifu yanasema kwamba, Imani inapata chimbuko lake kwa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, kiasi kwamba, Biblia inapaswa kuwa ni Maktaba ya kwanza kabisa kuwamo ndani ya Familia ya Kikristo, ili familia hizi ziweze kuonja uwepo endelevu wa Yesu Kristo mkombozi wa dunia katika maisha na vipaumbele vyao. RealAudioMP3

Kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya kifamilia kuna maanisha ujenzi wa mchakato wa kurithisha imani inayofumbatwa katika ukimya wa Mwenyezi Mungu aliyefunuliwa na Yesu Kristo. Hii ndiyo changamoto ambayo imetolewa na washiriki wa Vyama vya Biblia kutoka sehemu mbali mbali za dunia, katika mkutano wao uliokuwa unafanyika mjini Roma, ukiongozwa na kauli mbiu “Biblia katika familia”.

Mapokeo ya Kanisa yanaonesha kwamba, usomaji, tafakari na umwilishaji wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya kifamilia ni kati ya vipaumbele vya shughuli na mikakati ya kichungaji. Hii ni changamoto iliyotolewa na Mababa wa Kanisa kama vile Mtakatifu Yohane Krisostom, aliyewahimiza waamini kuhakikisha kwamba, wanavalia njuga usomaji wa Biblia katika Familia.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia anasema, kati ya “majanga yanayoziandama Familia nyingi za Kikristo ni kudhani kwamba, Maandiko Matakatifu yanasomwa tu wakati wa Ibada ya Misa, Jumapili na Siku kuu zilizoamriwa. Watu wenye hekima waliwahi kusema kwamba, dunia inasimikwa katika nguzo kuu tatu: Biblia, Liturujia na Matendo ya huruma. Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, imekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kutafakari Neno la Mungu, kuimarisha imani na hatimaye, kumwilisha Neno hili katika uhalisia wa maisha.

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, umeliwezesha Kanisa kuwarudishia tena waamini Biblia mikononi mwao, ili Neno la Mungu liweze kuwa ni dira na mwanga katika hija ya maisha yao hapa duniani. Hii ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza waamini kujitaabisha: kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, wakianzia kwenye Familia, Jumuiya Ndogo Ndogo na kwenye Vyama vya Kitume Maparokiani.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia anasema, msisitizo huu umetolewa pia na Mababa wa Sinodi Maalum juu ya Neno la Mungu iliyofanyika hivi karibuni mjini Vatican kuhusu umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Washiriki wa Mashirikisho ya Vyama vya Biblia, Kitaifa, Kikanda na Kimataifa wameendelea kukazia katika mkutano wao kwamba, kuna haja kwa Kanisa kuhakikisha kwamba, waamini wanajenga utamaduni wa kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume wao.

Wajumbe hao wanasikitika kusema kwamba, kwa bahati mbaya, Neno la Mungu si nguzo na mwanga thabiti katika maisha ya kiroho ya waamini walio wengi katika ulimwengu mamboleo, kinyume kabisa na Mapokeo ya Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliwahi kuwaambia vijana kuhakikisha kwamba, wanajenga uhusiano wa dhati kati ya Maandiko Matakatifu, Ndoa na Familia na kwamba, maisha yao yanapaswa kuonesha Mpango wa Mungu katika Ndoa na Familia. Waamini wajenge utamaduni wa kuwa waaminifu kwa Neno la Mungu na kati yao wenyewe, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, Mungu ana mpango maalum katika maisha yao. Hizi ni juhudi za kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Tafakari makini ya Neno la Mungu inaweza kuwapatia mwanga wa imani na matumaini wanafamilia katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kuna uhusiano wa pekee kati ya Neno la Mungu, Kanisa na maisha ya Ndoa na Familia, ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza Wanandoa kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa kuwalea watoto wao kadiri ya imani na mafundisho ya Kanisa, kwani wao kimsingi ni watangazaji wa kwanza wa Neno la Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu.

Bila ya wazazi na walezi kutekeleza barabara wajibu wao ndani ya familia, itakuwa vigumu kuweza kurithisha imani kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifumstaafu Benedikto wa kumi na sita, anazialika Jumuiya za Kikristo, kuhakikisha kwamba, zinasaidia familia kutekeleza wajibu wake wa kulea watoto katika misingi ya imani na Mafundisho ya Kanisa.

Familia zijenge utamaduni wa kusali, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu katika maisha yao ya kila siku. Wazazi na walezi wawajengee watoto wao uwezo wa kutamani na kusoma Biblia Takatifu. Biblia iheshimiwe na kutunzwa vyema. Jitihada hizi ziendelezwe pia katika Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo. Wanawake wa Kikristo wakipania kwa moyo na akili zao zote, wanaweza kuwa kweli ni vyombo makini vya kuhamasisha usomaji na tafakari ya Neno la Mungu katika familia za Kikristo.

Familia zijitahidi kuwa na Biblia Takatifu katika mazingira yao. Inawezekana kabisa kuwa na Biblia Takatifu katika lugha anayoifahamu mwamini. Biblia ni Kitabu mahususi cha sala na maisha ya Kikristo. Juhudi zinaendelea kufanyika ndani ya Kanisa ili kuhakikisha kwamba, hata vyama vya kitume kwa watoto na vijana vinajenga utamaduni wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu, kwani mwelekeo huu unalenga kumjenga mtu mzima: kiroho na kimwili.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia kwamba, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, itakuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha, ili hatimaye, familia hizi ziweze kuwa kweli ni wadau wa Uinjilishaji Mpya.

Makala haya yamehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.