Tanzania yanadiwa kwa Wachina katika sekta ya Utalii
Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amewaeleza washiriki wa Maonesho 14 ya Kimataifa
ya China Magharibi kuwa Tanzania ni nchi ya pili duniani na ya kwanza katika ukanda
wa Afrika Mashariki kuwa na vituo vingi vya utalii na akawataka waanze kumininika
kwa wingi kuja nchini kutalii.
Ametoa mwaliko huo Jumatano, Oktoba 23, 2013
wakati akihutubia kwenye maonesho hayo ya kimataifa yanayojulikana kama 14th Western
China International Fair yaliyoanza leo jijini Chengdu kwenye jimbo la Sichuan, China
na kuhudhuriwa na mataifa mbalimbali.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa miongoni mwa
viongozi wa mataifa 11 waliopata fursa ya kuhutubia maonesho hayo makubwa ya kimataifa,
aliziomba kampuni za China kuja nchini kuwekeza kwa kujenga viwanda vingi vya nguo
zinazotokana na zao la pamba.
Alitumia fursa hiyo pia kuinadi Tanzania kuwa
ni nchi yenye ardhi kubwa tena yenye rutuba ambayo inafaa kwa kilimo, na kuzisihi
kampuni za Kichina ambazo zinataka kuwekeza kwenye sekta ya kilimo zije nchini kwa
ajili ya kulima kilimo cha mashamba makubwa ya biashara.
Katika hotuba yake,
Waziri Mkuu Pinda aliwaambia wawakilishi wa kampuni mbalimbali za kimataifa zinazoshiriki
kwenye maonyesho hayo kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazolima pamba kwa wingi
wakati China ni taifa ambalo limebobea kwa viwanda.
“Sisi tuna pamba na
ninyi mna viwanda, nawaomba mje nchini kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya nguo
kwani malighafi ipo ya kutosha,” alisema. Maonesho hayo yanashirikisha kampuni 4,000
kutoka nchi 72 mbalimbali ulimwenguni na majimbo mengine ya hapa China.
Ufunguzi
wa maonesho hayo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi saba, mawaziri wakuu wanne mbalimbali
akiwemo Pinda, mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi 25, wakuu wa mashirika ya kimataifa
wapatao tisa na mabalozi wanane wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini China.
Gazeti
la Serikali la China Daily limeyaelezea maonesho hayo kuwa ni makubwa kufanyika katika
jimbo hilo na inatarajiwa kuwa mikataba yenye thamani ya dola za Marekani bilioni
82 itasainiwa na kampuni mbalimbali.
Akizungumzia kuhusu utalii, Waziri mkuu
pia alitumia fursa hiyo ya kuhutubia maonesho hayo makubwa ya kimataifa kuinadi Tanzania
katika sekta ya utalii na kuwaeleza wafanyabiashara hao Tanzania ni nchi ya pekee
katika ukanda wa Afrika Mashariki yenye vivutio vingi vya utalii vikiwemo vitatu vilivyoko
kwenye maajabu saba ya Afrika.
“Kati ya maajabu saba mapya ya asili barani
Afrika, yaliyotangazwa Februari, mwaka huu, maajabu matatu yako nchini mwetu ambayo
ni mlima Kilimanjaro, hifadhi ya Serengeti na Bonde la Ngorongoro,” alisema na kuongeza
kuwa pamoja na vivutio hivyo lukuki lakini bado idadi ya watalii wanaofika nchini
kutoka China haijawa ya kuridhisha.
Alisema licha ya maajabu hayo matatu, lakini
pia kuna hifadhi nyingine za wanyama, hifadhi za mambo ya kale na kisiwa maarufu cha
Zanzibar. Alisema hata takwimu za kimataifa zinaitaja Tanzania kama nchi ya pili duniani
yenye vivutio vingi kuliko nchi zingine ikiifuatia Brazil ambayo inaongoza kwa vivutioa
duniani.
“Pamoja na vivutio hivi lakini idadi ya watalii kutoka China bado
ni ndogo, sasa nawaambieni njooni kwetu mjionee maajabu ya dunia,” alisema. Mkutano
huo ulihutubiwa na viongozi saba kutoka mataifa mbalimbali ambao wote walieleza kunufaika
na uhusiano wa kibiashara na China.
Viongozi hao ni magavana wakuu ambao ni
Quentin Bryce wa Australia na David Johnston wa Canada. Wengine ni Rais wa Macedonia,
Gjorge Ivanov, Waziri Mkuu wa Mongolia, N. Altanhhuyag, Naibu Waziri Mkuu wa Berarus,
Analy Tozik, Waziri Mkuu wa zamani wa Ufaransa, Jean-Pierre Raffarin na Mwakilishi
wa Umoja wa Mataifa, Jan Mattassons.
Kwa upande wa Ardhi, Waziri Mkuu alisema
Tanzania bado ina ardhi kubwa ambayo haijaguswa kwa kilimo, hivyo kampuni za China
na zingine za mataifa mengine yanayoshiriki kwenye maonesho hayo kuja kuwekeza nchini
hasa katika sekta ya kilimo.
Waziri Mkuu alisema, anatoa ukaribisho kwa kampuni
hizo kwa vile Tanzania sera yake ya kibiashara ni ya kushirikiana na mataifa mengine
na kukaribisha wawekezaji wa nje na wa ndani kuja kuwekeza nchini katika maeneo ambayo
wanaona inafaa kufanya hivyo.
“Maonesho haya ni ishara kwamba China inatoa
fursa mbalimbali kwa watu wa ndani na nje ya nchi kufanya biashara pamoja, na sisi
tuna sera ya namna hii hivyo tunawakaribisheni kuja nchini kuwekeza kwa wingi,” alisema
Pinda.
Alisisitiza pia kuwa wawekezaji hao wanaweza kuja kuwekeza katika sekta
kama ya gesi ambayo imegundulika hivi karibuni au kwenye makaa ya mawe na hata kwenye
madini ya chuma. “Ndiyo maana nasema kampuni za China njooni muwekeze kwetu hasa katika
sekta hizi.”
Waziri mkuu ambaye alistaajabishwa na maonesho hayo ya kijimbo
ambayo ni makubwa na yenye mvuto kwa kampuni kubwa duniani, alitoa mwito kwa kampuni
za China kuja kushiriki kwenye maonesho ya kibiashara ya kimataifa ya mwakani ambayo
yatafanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 8, 2014.
Waziri mkuu jana ameondoka
Chengdu na kueleka katika jimbo la Guangzhou ambako atamalizia ziara yake ya sikua
tisa ya kikazi.