Nguvu ya neema: udumifu wa ndoa na majadiliano kuhusu wanandoa walioachana kuhusu
kupokea Sakramenti za Kanisa
Baba Mtakatifu Francisko ametangaza Maadhimisho ya Sinodi Maalum kwa ajili ya Familia
itakayofanyika mwezi Oktoba 2014, ili kuangalia kwa makini changamoto za kichungaji
zinazoikabili familia katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kati ya masuala tete yanayozikabili familia nyingi ni wanandoa walioachana
na kuamua kuoa au kuolewa tena. Askofu mkuu Gerhard Ludwig Muller, Mwenyekiti wa Baraza
la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa analiangalia kwa utulivu kabisa suala hili
tete katika makala iliyochapishwa kwenye Gazeti la L'Osservatore Romano, linalomilikiwa
na Vatican.
Kwanza kabisa analichambua tatizo hili katika misingi ya Maandiko
Matakatifu, tangu Agano la Kale hadi Agano Jipya na changamoto zilizojitokeza wakati
huo, hadi pale Yesu mwenyewe alipotoa msimamo thabiti kuhusu ndoa kadiri ya mpango
wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Udumifu wa maisha ya ndoa ni agizo la Kristo
mwenyewe linalofafanuliwa na Mtakatifu Paulo katika nyaraka zake mbali mbali.
Muungano
kati ya mwanaume na mwanamke aliyebatizwa ni Sakramenti ya ndoa ambayo inadumu maisha
yote mintarafu mpango wa Fumbo la Maisha ya Kanisa, kwani hiki ni kielelezo cha upendo
mkamilifu ambao unapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo mwenyewe. Muungano kati ya
Bwana na Bibi katika kifungo cha upendo wa ndoa, kinawajalia waamini hao neema na
baraka katika maisha yao.
Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki inafafanua kwamba,
agano la ndoa, ambalo kwa njia yake, mwanaume na mwanamke huunda kati yao Jumuiya
kwa maisha yao yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili ya mafaa yao na kwa ajili
ya kuzaa na kulea watoto. Agano hili kati ya wabatizwa, limeinuliwa na Kristo Bwana
kwa hadhi ya Sakramenti.
Askofu mkuu Muller anaiangalia Sakramenti ya Ndoa
kadiri ya Mapokeo ya Kanisa, kwa kukazia umuhimu wa kuheshimu na kuthamini Maandiko
Matakatifu na mafundisho ya Mababa wa Kanisa kuhusu udumifu wa ndoa ya Kikristo. Kwa
wanandoa ambao walikuwa wameachana na wenzi wao wa ndoa walikuwa hawaruhusiwi kupokea
Sakramenti za Kanisa. Suala hili lilikuwa ni tete wakati fulani katika historia ya
Kanisa kiasi kwamba, kuna baadhi ya nchi ziliamua kujitenga na Khalifa wa Mtakatifu
Petro kutokana na msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu udumifu wa Sakramenti ya Ndoa.
Umuhimu
wa wanandoa kudumu katika maagano yao ni jambo ambalo pia limepewa kipaumbele cha
pekee na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa
Pili aliyelitaka Kanisa kutoa huduma za kiroho kwa wanandoa walioachana na kuamua
kuoa au kuolewa tena Kiserikali. Lakini, Sakramenti ya Ndoa kwa upande wa Kanisa bado
inaendelea kuwafunga wanandoa hao.
Ni waamini wanaopaswa kushiriki kikamilifu
katika maisha na utume wa Kanisa, lakini hawatarusiwa kupokea Ekaristi Takatifu, kielelezo
cha upendo na uaminifu wa Kristo kwa Kanisa lake. Lengo ni kuendelea kuonesha umuhimu
wa Sakramenti ya Ndoa kadiri ya Mafundisho ya Kanisa bila mkanganyiko wowote. Wanandoa
walioachana na kuoana au kuolewa tena, hawawezi pia kupokea Sakramenti ya Upatanisho.
Hakuna mabadiliko yanayoweza kufanywa kwa kuangalia hali za wanandoa husika.
Kumbe,
wanandoa hawa wanapaswa kuongozwa na dhamiri nyofu. Sababu za kuvunjika kwa ndoa zinaangaliwa
na taasisi za Kanisa zinazoshughulikia mausla ya ndoa na familia kadiri ya sheria
za Kanisa. Hapa hakuna ubaguzi wa Kisakramenti bali ni uaminifu kwa Kristo na Kanisa
lake. Kanisa linaendelea kuonesha masikitiko yake kutokana na mpasuko huo ambao unasababisha
machungu katika maisha ya wanandoa waliotengana, lakini hata hivyo wanashauriwa kuendelea
kujisikia kuwa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa.
Hii ni kutokana na
ukweli kwamba, upendo wa Kristo hauna ubaguzi kwa mtu awaye yote! Ni wajibu wa Jumuiya
za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinawasaidia wanandoa hawa kuanza mchakato wa toba,
wongofu wa ndani na upatanisho.
Askofu mkuu Muller anasema, uamifu kati ya
wanandoa ni jambo la muhimu sana katika mahusiano yao ndani ya ndoa na familia. Ni
mwaliko wa kusaidiana ili kuvuka vikwazo na "majanga" yanayozinyemelea familia zao;
wasimame kidete kuwalea na kuwahudumia watoto wao ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa
Mwenyezi Mungu. Watoto ndio wanaoathirika kwa kiasi kikubwa pale wazazi wao wanapoamua
kuvunja maagano ya ndoa yao. Wanandoa wakumbuke daima kwamba, kile ambacho Mungu ameunganisha,
mwanadamu hana ruhusa ya kukitenganisha.
Hizi zote ni changamoto za maisha
ya ndoa na familia, zinazopaswa kufanyiwa kazi na kupatiwa majibu muafaka kadiri ya
Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa. Kuna sababu ambazo hata Kanisa lenyewe linazipatia
uzito wa pekee hata kuruhusu ndoa iweze kuvunjwa, lakini maagano ya ndoa iliyoadhimishwa
Kanisani kwa kufuata sheria na kanuni za Kanisa bado ina umuhimu wa pekee mbele ya
Mwenyezi Mungu. Viongozi wa Kanisa na Jumuiya za Kikristo wawasaidie wanandoa wanaopambana
na magumu katika maisha yao ili waweze kuyakabili magumu haya kwa imani, matumaini
na moyo mkuu.
Askofu mkuu Muller anasema, kuna mawazo kwamba, wanandoa walioachana
na kuoa au kuolewa tena waruhusiwe kupokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, wakiongozwa
na dhamiri nyofu, wazo ambalo lilikwishakataliwa na Kanisa. Hii inatokana na ukweli
kwamba, ndoa si jambo la uhusiano wa upendo kati ya wanandoa mbele ya Mwenyezi Mungu,
bali ni Sakramenti ya Kanisa na ushuhuda wa imani.
Sakramenti ya ndoa haina
budi kujikita katika ukweli na kwamba, huu ni utekelezaji wa sheria ya Mungu na wala
Kanisa halina mamlaka ya kwenda kinyume na sheria hii. Katika mambo yote haya huruma
ya Kristo inapewa kipaumbele cha pekee kwa wanandoa wanaokabiliana na magumu katika
mahusiano yao, lakini hata hapa kuna ugumu katika mafundisho ya Kanisa yanayokazia:
utakatifu na haki.
Huruma ya Mungu si tiketi ya kuvunja amri za Mungu na za
Kanisa. Lakini ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu inampatia mwamini neema ya kutubu
na kuongoka baada ya kutopea katika lindi la dhambi na mauti, ili kuanza tena hija
ya maisha mapya kadiri ya sura na mfano wa Mwenyezi Mungu. Mama Kanisa ataendelea
kuwasindikiza wanandoa waliotengana, wakaoa au kuolewa tena katika mchakato wa uponyaji
wa ndani na wokovu. Kuzuiliwa kwao kupokea Sakramenti za Kanisa ni kielelezo makini
cha udumifu wa kiapo cha ndoa hadi kifo kitakapowatenganisha.
Wanandoa hawa
wanapaswa kusaidiwa kwa mapana zaidi badala ya kuliangalia tatizo hili katika jicho
la Sakramenti ya Ekaristi Takatifu peke yake. Kuna njia mbali mbali ambazo mwamini
anaweza kuzitumia ili kujenga uhusiano wake na Mwenyezi Mungu kwa kuimarisha: imani,
matumaini na mapendo. Waamini wajenge na kukoleza moyo wa toba na wongofu wa ndani;
matendo ya huruma na moyo wa sala.
Mwenyezi Mungu anazo njia nyingi za kuonesha
uwepo wake kwa waja wake kwani huruma na upendo wake havina mipaka. Ni jukumu kwa
Jumuiya za Kikristo kuonesha moyo wa ukarimu, huruma na mapendo kwa wanandoa wanaoogelea
katika shida na magumu ya maisha yao ya kiroho, ili wao pia waweze kuonja huruma na
upendo wa Kristo mchungaji mwema. Kanisa linapenda kutoa huduma makini kwa wanandoa
hawa, huduma ambayo inasimikwa katika ukweli na upendo.
Taarifa hii imehaririwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.