2013-10-23 11:12:28

Jitahidini kutafuta haki inayojikita katika upatanisho na matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 23 Oktoba 2013, amewapongeza wahudumu wa maisha ya kiroho wanaotekeleza utume wao magerezani katika mazingira magumu, kuhakikisha kwamba, wanawafikishia wafungwa salam na matashi mema kutoka kwake.

Anasema anawakumbuka katika maisha na sala zake, ili waweze kuwahudumia wafungwa kwa ari na moyo wa Kristo mchungaji mwema. Hata katika mazingira kama haya, Yesu bado anaendelea kufanya hija pamoja nao, ili hatimaye, waweze kutubu, kuongoka na kuanza maisha mapya.

Baba Mtakatifu anasema, hata leo hii Yesu bado yuko kifungoni kutokana na ubinafsi, mifumo mibaya ya maisha, ukosefu wa misingi thabiti ya haki na amani na kwamba, katika ulimwengu wa mwenye nguvu mpishe, wanyonge ndio wanaoendelea kuteseka zaidi magerezani. Wafungwa watambue kwamba, Yesu ni mwenza wa mateso na mahangaiko yao magerezani na kwamba, upendo wake unawafikia wote pasi na ubaguzi.

Baba Mtakatifu anasema, hata wakati huu bado anaendelea kuwasiliana na baadhi ya wafungwa aliowafahamu alipokuwa Jimbo kuu la Bueno Aires. Akipata nafasi huwapigia simu na kuzungumza nao kama njia ya kuwaonjesha tone la upendo wa Kristo na ni nafasi ya kufanya tafakari ya kina kuhusu wafungwa walioko magerezani. Utume na maisha yake kama Askofu unamwajibisha kusali na kuwaombea wafungwa kama njia ya kuonesha uwepo wa Kristo katika maisha yao, licha ya kuendelea kuwa magerezani.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, utume wa maisha ya kiroho magerezani si lelemama unahitaji moyo wa sadaka na uvumilivu, lakini pia ni kielelezo cha matendo ya huruma na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hawa ni watu wanaohitaji haki inayojikita katika upatanisho na matumaini makubwa zaidi.

Hii inatokana na ukweli kwamba, mwanadamu ni dhaifu, kuna vishawishi vingi na Shetani anaendelea kuwateka wanadamu kwa njia mbali mbali, kumbe haki inayojikita katika matumaini ni jambo linalowezekana. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume, wao na wale wanaowahudumia magerezani.

Zaidi ya Mapadre 150 kutoka sehemu mbali mbali za Italia wako mjini Roma kuhudhuria kongamano la kitaifa kwa ajili ya wahudumu wa kiroho magerezani. Kongamano hili linaongozwa na kauli mbiu "Huru kwa ajili ya kuwaweka wengine huru. haki, adhabu au upatanaisho". Hii ni mada inayogusa hali halisi ya magereza nchini Italia, magereza ambayo kwa sasa yamefurika kupita uwezo wake wa kawaida. wajumbe hao wamepokea pia ujumbe kutoka kwa viongozi mbali mbali wa Serikali ya Italia.

Viongozi hawa wa kiroho wanapaswa kukabiliana na hali ya magereza kama alivyofanya Kristo mwenyewe pale Msalabani, kwa kuwajalia wafungwa wanaowahudumia wokovu na mabadiliko katika maisha yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.