2013-10-22 14:34:56

Serikali ya Tanzania kuboresha usafiri wa maji: Ziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni aibu kwa Serikali kudaiwa na wakulima na amewahakikishia wakulima wa Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe, kuwa watalipwa haraka iwezekanavyo fedha zao wanazodai kwa kuiuzia Serikali mahindi yao.

Aidha, Rais Kikwete amethibitisha kuwa meli ambazo Serikali yake iliahidi kununua kwa ajili ya usafiri katika maziwa makuu ya Tanzania zinajengwa na zitazinduliwa kabla ya mwaka 2015, zinaweza kuwa meli mbili badala ya moja kwa kila moja ya maziwa ya Nyasa, Tanganyika na Victoria.

Rais Kikwete ameyasema hayo, Jumatatu, Oktoba 21, 2013, wakati alipozungumza kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya Wilaya ya Ludewa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Njombe.

Rais Kikwete amewaambia wakazi wa Ludewa kwenye mkutano wa hadhara kuwa ni kweli kuwa Serikali yake inadaiwa kiasi cha Sh.bilioni 17 ikiwa ni deni la wakulima wa mikoa mbali mbali nchini ambao waliuza mahindi yao ya msimu uliopita kwa kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Suala hilo lilijirudia tena wakati Rais Kikwete alipokuwa anapokea Ripoti ya Maendeleo ya Wilaya ya Ludewa ambako ameambiwa kuwa wakulima wa Wilaya hiyo pekee walikuwa bado wanaidai Serikali Sh.bilioni 3.115 ambayo ni thamani ya mahindi tani 6,231 ambayo wakulima hao waliiuzia NFRA.

Rais Kikwete ameambiwa kuwa mpaka sasa wakulima wa Wilaya ya Ludewa wamelipwa kiasi cha Sh.bilioni 2.839 kutokana na tani za mahindi tani 5,679. NFRA ilikuwa imelenga kununua kutoka kwa wakulima wa Wilaya ya Ludewa kiasi cha tani 13,000 lakini mpaka sasa imeweza kununua tani 11,911 ingawa sehemu kubwa ya kiasi hicho hakijalipiwa na Serikali.

“Hii ni aibu. Serikali haiwezi kudaiwa na wakulima. Hizi fedha zitalipwa tu,” amesema Rais Kikwete na kuelezea hatua ambazo amezichukua binafsi katika siku mbili kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao. Rais Kikwete pia amesema kuwa Serikali yake itaangalia uwezekano wa kununua tani 2,972 za mahindi ya msimu uliopita zilizobakia mikononi mwa wakulima wa Wilaya hiyo.

“Naambiwa kuwa bado NFRA inahitaji kiasi cha tani 40,000 hivi ili kukamilisha shehena ya idadi ya kiasi cha tani 250,000 za mahindi kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa mwaka huu. Nitawaambia waangalie kama wanaweza kununua kiasi hiki kilichobakia mikononi mwa wakulima wa Ludewa.”

Kuhusu maombi ya wananchi wa Ludewa kununua meli ya kuchukua nafasi ya Mv. Mbeya iliyozama katika Ziwa Nyasa ili kurahisisha usafiri ndani ya Ziwa hilo ambalo linapakana na Wilaya ya Ludewa, Rais amesema kuwa Serikali yake inanunua meli hiyo. “Tunajua kuwa meli ya Mv. Mbeya ilizama katika Ziwa Malawi na kwa kweli meli zimezama katika maziwa mengine makubwa ya Tanganyika na Victoria, na mimi kwenye Kampeni niliahidi kuwa nitanunua meli moja kwa kila ziwa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Tumeagiza meli tatu kutoka Korea Kusini. Zinajengwa. Tumeagiza meli nyingine tatu kutoka Denmark. Nazo zinajengwa. Hivyo, tunaweza kupata siyo meli moja bali meli mbili katika maziwa yote matatu. Ni matumaini yangu kuwa nitaweza kuzizindua meli hizo kabla ya kumaliza kipindi changu cha uongozi, mwaka 2015.”

Rais Kikwete pia amefafanua kuhusu kero nyingine zilizoibuliwa na wakazi wa Wilaya ya Ludewa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa daraja kwenye Mto Ruhuhu ambao amesema litajengwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.