2013-10-22 09:04:51

Mwaka wa Imani kimekuwa ni kipindi cha neema, mshikamano na mwamko wa kimissionari!


Mama Kanisa anapojiandaa kufunga rasmi Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, Kanisa Katoliki nchini Pakistan linalisema, Mwaka wa Imani, umeacha utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa nchini humo. Waamini wengi wameonesha mwamko mpya kuhusiana na utume na maisha ya Kanisa.

Umekuwa ni fursa ya kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa waamini wenyewe pamoja na majirani zao, hasa pale walipokabiliana na madhulumu pamoja na changamoto za maisha ya kila siku. Ni mwaka ambao pia Kanisa nchini Pakistan limeendelea kushuhudia madhulumu na nyanyaso za kidini dhidi ya Wakristo na kwamba, bado wanaendelea kukumbuka mauaji ya Peshwar.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu Sebastian Francis Shaw, Msimamizi wa kitume, Jimbo kuu la Lahore, nchini Pakistan, kama sehemu ya Maandalizi ya kufunga Mwaka wa Imani, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 87 ya Kimissionari Duniani, iliyoadhimishwa na Mama Kanisa jumapili iliyopita.

Mwaka wa Imani imekuwa ni fursa kwa waamini kujikita zaidi katika katekesi na majiundo endelevu kuhusu: imani yao kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na maisha ya uzima wa milele. Waamini wamejitaabisha kumfahamu Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, kiini na chemchemi ya imani yao. Waamini wameguswa na uwepo endelevu wa Kristo katika hija ya maisha yao ya kiroho kwa njia ya Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, maisha adili na sala.

Kwa maneno machache, waamini wamejitahidi kumwilisha katika safari yao ya kiroho: Imani, Sakramenti, Amri za Mungu na Sala, mambo msingi yanayofafanuliwa kwa kina na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, ambayo Mama Kanisa ameadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu ilipochapishwa kwa mara ya kwanza na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili. Ni matumaini ya Kanisa Katoliki nchini Pakistan kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yatawakirimia waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo matunda ya haki, amani, upendo na mshikamano.

Viongozi mbali mbali wa kidini waliohudhuria tukio hili la kidini na kiekumene, wamekiri kwamba, imani kimsingi inapaswa kuwa ni kiungo kikubwa miongoni mwa waamini wa dini na madhehebu mbali mbali, lakini kwa bahati mbaya, imani imekuwa pia ni chanzo cha mpasuko na kinzani za kidini sehemu mbali mbali za dunia. Licha ya changamoto hii ya ujenzi wa majadiliano ya kidini na kiekumene, waamini wa madhehebu mbali mbali wameendelea kutoa ujumbe wa haki, amani, upendo, mshikamano na matumaini kwa wananchi wa Pakistan katika ujumla wao.

Ufunguzi wa Mwaka wa Imani nchini Pakistan, ulihudhuriwa na viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali nchini humo. Kwa pamoja, walijizatiti kuendelea kushirikiana katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu; kwa kujikita zaidi katika mambo yale yanayowaunganisha na kuyaepuka yale yanayowachefua na kuwagawanya kama wananchi wa Pakistan. Walijiwekea azimio la kuendelea kukutana na kusali kwa pamoja kama njia ya kuimarisha malengo ya pamoja kwa ajili ya mafao ya wengi.








All the contents on this site are copyrighted ©.