2013-10-22 08:53:40

Jumuiya ya Kimataifa, sikilizeni kilio cha wananchi wa Afrika ya Kati!


Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui ambaye pia ni Rais wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Caritas anasema kwamba, kwa sasa hali ya wananchi wengi nchini humo inaendelea kuwa tete kutokana na machafuko ya kisiasa, kiasi kwamba, kuna uvunjaji mkubwa wa haki msingi za binadamu unaofanywa na wanajeshi wa Seleka waliojitwalia madaraka mwezi Marchi, 2013.

Wanajeshi wa Seleka wanaendelea kutuhumiwa kwa kujihusisha na vitendo vya mauaji ya kinyama, ubakaji, ujambazi na watu wengi wamechomewa nyumba zao, shutuma ambazo zimetolewa taarifa na wadau mbali mbali, lakini hakuna hatua za kinidhamu zilizochukuliwa na Serikali hadi sasa.

Kutokana na hali kama hii, Askofu mkuu Nzapalainga yuko mjini Geneva, ili kuwajulisha wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva na Mashirika ya Kimataifa kuhusu uvunjwaji mkuu wa haki msingi za binadamu Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Kanisa nchini humo linautaka Umoja wa Mataifa kuimaarisha uwezo wa Majeshi ya kulinda amani kutoka Umoja wa Afrika, ili wananchi waweze kuwa na uhakika wa maisha na usalama wao.

Idadi ya Wanajeshi wa Seleka imeongezeka kutoka wanajeshi 3,500 waliokuwepo mwezi Marchi hadi kufikia wanajeshi 25,000 kwa sasa. Kati ya wanajeshi hawa kuna idadi kubwa ya watoto ambao wanalazimishwa kujiunga na jeshi hilo. Idadi ya silaha ndogo ndogo inazidi kuzagaa miongoni mwa wananchi kiasi kwamba, watu wengi hawana tena uhakika wa usalama wa maisha yao.

Zaidi ya nyumba 2,000 zimechomwa moto na familia zilizokuwa zinaishi humo zimelazimika kutafuta makazi kwenye taasisi za kidini. Caritas inaendelea kutoa msaada wa hali na mali, lakini kwa sasa hali hii inatisha. Viongozi wa kidini wanaendeleza mchakato wa msamaha na upatanisho ili kujenga misingi ya haki, amani na utulivu, mambo msingi kwa maendeleo endelevu ya watu.








All the contents on this site are copyrighted ©.