2013-10-21 11:36:36

Tamaa ya fedha na mali ni chanzo cha majanga mengi duniani!


Baba Mtakatifu Francisko amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiadhari na ulafi wa fedha ambao unaweza kuwa ni chanzo cha kinzani, migogoro na majanga katika ngazi ya mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake. Fedha inapaswa itumike vyema kwa ajili ya kusaidia mchakato wa maendeleo ya mtu mzima kiroho na kimwili na wala si vinginevyo.

Tamaa ya fedha inaweza kumsababishia mtu kuiona fedha kama mungu wake mdogo. Mtakatifu Paulo anawakumbusha waamini kwamba, Yesu Kristo aliyekuwa ni tajiri wa mambo mengi, lakini hakuona kwamba utajiri huo ni kitu cha kung'anganyia sana, akajishusha ili aweze kumtajirisha mwanadamu. Kwa maneno mengine, Mwenyezi Mungu amejinyenyekesha ili aweze kuwahudumia wanadamu.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 21 Oktoba 2013. Anawataka waamini kuwa macho na matumizi ya fedha, daima wakiweka matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu. Tamaa ya fedha na mali ni chanzo cha majanga mengi duniani, hali ambayo inakwamisha pia mshikamano wa kidugu miongoni mwa watu.

Yesu anawafundisha waamini kutembea katika njia ya ufukara kama njia ya waamini ya kutoa kipaumbele cha pekee kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, maisha na mtu hayategemei wingi wa mali au fedha aliyo nayo.







All the contents on this site are copyrighted ©.